Habari Mseto

Waumini washtuka pasta wao kupigwa risasi kwa madai ya kuwa jambazi sugu

April 9th, 2024 2 min read

NA KITAVI MUTUA

WASHIRIKA wa kanisa moja katika Kaunti ya Kitui, ambalo pasta wake alipigwa risasi na polisi kwenye kwa dai la kuhusika katika kisa cha wizi wa mabavu, bado wako katika hali ya mshangao, kuhusiana na tukio hilo.

Kwenye mahojiano, washirika wa kanisa la Open Heaven City Chapel, lililo katika eneo la Soweto, Kitui, walimtaja pasta huyo kama mtu aliyekuwa mwangalifu sana kimienendo.

Pasta huyo, aliyetambuliwa kama Bw Ezekiel Muinde Mwangangi, alionekana kama mtu mnyenyekevu na aliyependa Mungu.

“Sote tuko katika hali ya mshangao. Alikuwa miongoni mwa mapasta waliokuwa wametwikwa majukumu ya uongozi katika kanisa hili. Ndiye alikuwa amepewa jukumu la kusimamia tawi jipya la kanisa hili katika soko la Kauma, Kitui Magharibi,” akasema Bw Ambrose Wambua, mshirika mwenye duka la kuuza bidhaa tofauti katika soko la Soweto.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Wambua, alisema kwamba hawakuwa na jambo lolote lililowafanya kumshuku pasta huyo. Alianza kuhudumu katika kanisa hilo mapema mwaka uliopita.

“Ndiye alikuwa akihubiri karibu kila mikutano ya injili ya kanisa letu. Alikuwa amejijengea jina na sifa ya mhubiri kamili wa injili,” akasema Bw Wambua.

Alisema maombi yao ni kwamba asingeuawa, ili apate nafasi ya kueleza yale aliyoyajua mahakamani.

Pasta huyo, ambaye hakutambulika mara moja katika eneo la wizi huo, alikuwa miongoni mwa genge lililovamia duka la jumla linalomilikiwa na Bw Muli Munyoki wiki iliyopita na kumnyang’anya kwa kumtishia kwa bunduki.

Wizi huo ulifanyika katika soko la Kavisuni, eneo la Kisasi.

Mshukiwa mwenzake—ambaye ni mshirika wa kanisa hilo—alitoroka akiwa na majeraha ya risasi. Hii ni baada ya polisi kuanza kuwafyatulia risasi.

Pasta David Munene, ambaye ndiye mwanzilishi wa kanisa hilo na aliyemwajiri marehemu, alisema amekuwa akihojiwa na polisi tangu kisa hicho kilipofanyika.

Amesisitiza kwamba hana uhusiano wowote na vitendo vya uhalifu vya pasta huyo nje ya kanisa.

Pasta Munene alisema kuwa marehemu alijiunga na kanisa hilo wakati wa mkutano wa maombi katika soko la Kalundu.

Alisema kwamba kama washirika wengine, aliendelea kujitolea kuhudumu hadi alipowasilisha ombi la kuruhusiwa kufungua tawi jingine katika eneo la Kauma.