Makala

Wauza bidhaa za plastiki mitandaoni kujiendeleza kielimu

September 3rd, 2019 4 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

@maggiemainah

Ukiwaona vijana wawili Bw Davis Oduor, 29 na Bi Mary Wanja, 21 wakipita na kukusanya chupa za plastiki katika jaa la Gioto na Mto Ndarugu zilizoko katika Kaunti ya Nakuru,utadhania pengine wamerukwa na akili. Lakini wana dhamira fulani.

Hawa ni wanafunzi wawili ambao dampo hili limekuwa ni lulu kwao kwa sababu huwapa malighafi ya kutengeneza bidhaa za maana kwa ajili ya matumizi.

Muhimu ni kwamba ni chanzo kizuri cha kipato kwao kwa sababu wanauza bidhaa wanazotengeneza.

Wawili hao ambao walisema walichoshwa kutafuta kazi za ofisini na zile zingine zinazochukuliwa kama za usafi.

Waliamua kutengeneza bidhaa za kutumika kama mapambo nyumbani. Ndio maana wanapotoka nyumbani mara nyingi hukusanya chupa za soda, maji au za juisi na dawa.

Wakishazikusanya chupa hizi, kwanza wanaziosha vizuri halafu kuzisuka ziwe kwa maumbo wayatakayo wao kabla ya kuzipaka rangi za kupendeza.

Wakishafanya hivyo, wanatumia gluu kuzishikanisha na kuzifanyia maumbo ya tofauti, ikiwa ni pamoja na kuweka vitufe vya shanga kwa chupa zenyewe.

Bila shaka matokeo yanakuwa ni chupa spesheli za kuweka maua na kutumika kama vikalio vya mishumaa ambavyo hupendeza machoni pa watu.

Hii ndiyo maana wanajishughulisha ili angalau kujitafutia riziki.

Oduor na Wanja walikutana kanisani ambako walielezana sababu na mazingira yaliyochangia wasiweze kuendelea na elimu baada ya kukamilisha ile ya kidato cha nne.

Ni hapo ndipo waliweka vichwa vyao pamoja ambapo bongo la biashara liliwajia.

Oduor ambaye alikulia mtaani Barnabas, Kaunti ya Nakuru anasema aliwahi kuitwa mwendawazimu na waliomuona akiokota chupa kandokando ya Mto Njoro na jaa la Gioto.

“Nilinyanyapaliwa na kuitwa chokoraa kwa sababu hakuna aliyejua mbona ninaamka saa kumi na moja asubuhi na kuanza kupekua kutoka jaa moja la hoteli hii hadi hiyo na vilevile kando ya mto na dampo,” anasema Oduor.

Alihisi kutengwa si tu na jamaa zake, bali pia na marafiki wa karibu.

Wachache waliosonga karibu naye walibakia kumshauri apate ushauri nasaha kwani waliona huko “aelekeako si kwema kabisa.”

Ilifika hatua ambapo wazazi nao wakishachoshwa na hali hii, walithubutu kumuambia kwamba si picha nzuri kwake kuonekana amebeba chupa chungu nzima zilizotiwa kwenye magunia.

Biashara hii yake alianzisha kwa mtaji wa Sh6,000 alizokuwa ameweka akiba wakati alikuwa akilipwa kama mhudumu wa wateja katika hoteli mojawapo ya mabasi ya Guardian.

Akianza utumiaji upya wa plastiki hizi kwa kutengeneza vyombo spesheli vya maua, lengo lake hasa lilikuwa ni kuhifadhi mazingira.

Lakini pia alianza kuona fursa ya kujiingizia pesa za kumkidhia mahitaji yake kuanzia malazi, chakula na mavazi.

“Nilitumia pesa za akiba kununua vitufe, gundi, rangi na nyororo. Kutokana na kazi yangu, ninapata kati ya Sh250 hadi Sh1000 kutegemea ukubwa wa chombo ninachotengeneza,” anasema kijana huyu.

Aidha, Bw Oduor aliyeanza kazi hii Aprili 2019, ameuza hadi vyombo 50 vya maua kwa mpangaji wa sherehe ya harusi aliyetumia bidhaa zake za Sanaa kama ‘centerpieces’ za kufanya mandhari ya harusi yawe ni ya kuvutia.

Kwa upande wake Bi Wanja yeye hutumia bidhaa za plastiki kutengeneza vivuli vya taa na glopu za umeme.

Yeye malighafi – chupa za plastiki – huyatoa katika soko la Wangige, Kaunti ya Kiambu.

Mwanadada huyu huuza bidhaa zake kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000 kulingana na ukubwa na muundo vilevile.

“Huwa sijali sana wanachofikiri watu, wala wanachosema. Ninajua ninachokitaka maishani na naishukuru familia na jamaa kwani wamekuwa wa msaada kwangu; mara zote wakinihimiza nizidi kutia bidii katika kazi hii,” anasema Bi Wanja.

Kwa pamoja wawili hawa wanasema vijana wengi wana maono na akili ya kufanya mazuri na kutengeneza vitu vya kupendeza, lakini wanakosa raslimali za kuwainua ili wafaulu maishani.

Wao hutumia mitandao ya kijamii kuzitafutia bidhaa zao soko na wanatarajia ipo siku watakuwa wameweka akiba kiasi fulani cha fedha kitakakachowawezesha kuendelea na elimu, zingatio likiwa ni sanaa.

“Pia tunawazia kufungua duka la bidhaa za sanaa na pia kuanza kuwapa mafunzo vijana wenzetu ili nao wapate njia halali za kujichumia mali pamoja na kujishughulisha na mikakati ya uhifadhi wa mazingira,” akasema Oduor

Kwa kweli chupa za plastiki zilizotupwa ovyo zimekuwa ni kero kubwa nchini Kenya kwa sababu mara nyingi mtu anapokunywa maji au juisi, chupa hizi huishia kuzagaa kotekote.

“Plastiki haiozi haraka; inaweza kuchukua miaka na mikaka. Lakini kwa kutumia chupa hizi kutengeneza bidhaa zingine, ina maana kwamba zinakuwa zinatumika kufanikisha majukumu mengine,” anasena Wanja.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya hivi majuzi inasema hadi chupa zaidi ya milioni moja inanunuliwa kila dakika kote ulimwenguni.

Hizi chupa huishia ziwani, katika mito na hata bahari na kusababisha madhara makubwa kwa si tu viumbe vya majini bali pia kwa mazingira kwa jumla. Katika nchi kavu chupa hizi zinazuia na kuziba mikondo ya maji na kusababisha maji yatuwame na kujenga mandhari ya mbu kuzaana.

Hii ina athari mbaya kwa afya ya mwanadamu. Utumiaji wa mara moja tu wa plastiki umesababisha kero kubwa ya bidhaa hizi.

Mwanaharakati wa mazingira Bw James Wakibia ambaye yuko mstari wa mbele kupinga matumizi ya chupa na mifuko ya plastiki anashikilia kwamba chupa aina hiyo ni adui kwa mazingira na hivyo ni afueni kubwa kuona vijana wanaovumbua njia mbadala za kuzitumia; hasa kupitia utengenezaji wa vyombo vya kuweka maua.

“Petco Kenya inafaa kuwawezesha watu aina hii kwa sababu hawa ndio wapenzi halisi wa mazingira safi na wapenda nchi hasa. Mifuko na bidhaa zingine za plastiki zinafunga mikondo ya mito na mabomba ya majitaka na hivyo kusababisha hali mbaya za kiafya,” anasema Bw Wakibia.

Bw Wakibia anaamini kwamba ili kuondokana na kero hii kabisa ipo haja ya serikali kuunda sheria na sera kuhusu udhibiti wa plastiki.

Anasema: “Ni muhimu pawepo depo kote nchini ili watumiaji bidhaa za plastiki kama chupa wanaweza kuzirudisha hata kama ni kwa kupewa angalau kiasi fulani cha pesa ili nazo zikatumike tena. Hatua kama hii itasaidia pakubwa.”