Wauzaji muguka washtaki kaunti

Wauzaji muguka washtaki kaunti

NA PHILIP MUYANGA

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa na bunge la kaunti hiyo, zimeshtakiwa na wafanyabiashara wa muguka kwa pendekezo la kuongeza ada ya leseni za biashara hiyo kwa asilimia 100.

Wafanyabiashara hao wanadai kuwa serikali hiyo inaendelea na mchakato wa kupitisha mapendekezo yao kwenye bajeti ya 2022/2023 bila kufuata sheria.

Kulingana nao, serikali hiyo pia inatekeleza mabadiliko hayo bila kujali maslahi wala maoni ya wadau wa biashara hiyo.

Wawakilishi wa Muungano wa Wauzaji Muguka kutoka Mbeere Kusini (MSMAE), Mabw Peterson Maina, Henry Mugambi na Laban Njiru, waliwasilisha maombi hayo mahakamani kwa niaba ya wafanyabiashara wenzao.

Wauzaji hao wa muguka wameeleza kuwa, Kaunti ya Mombasa ishawapa ilani ya kuchukua leseni mpya.

Wamelalamika hatua hii huenda ikaathiri biashara zao.

Wametaka mahakama itoe mwelekeo kuhusiana na kipengee cha 196 cha Katiba wanachosema kimelipa jukumu bunge la kaunti kuhusisha umma katika shughuli za kuandaa sera zake na shughuli nyingine.

Wameeleza kuwa, ada za kuendesha biashara hiyo zimekuwa zikiongezeka kwa muda, licha ya biashara zao kuathirika na janga la Covid-19.

“Washtakiwa wamegeuza suala hili kuwa la kisiasa. Serikali hiyo imeongeza ada ya kupata leseni ya kuuza muguka kwa kusudi la kudhibiti uuzaji muguka na kupuuza kuwa serikali ya kitaifa imetaja muguka kuwa mmea wa kilimo,” sehemu ya stakabadhi hizo inaeleza.

Wanaeleza kuwa, serikali ya kaunti hiyo iko katika mchakato wa kutekeleza masharti hayo ambayo bado hayajapitishwa. Wanataja hatua hiyo kama adhabu ambayo huenda ikawalazimu kufunga biashara zao.

“Walalamishi wana wasiwasi kuwa ongezeko la ada ya leseni iliyopendekezwa na Kaunti ya Mombasa inakiuka katiba na sheria kadhaa husika,” wakasema walalamishi.

Wanatafuta amri ya kuwa serikali ya kaunti, kupitia maajenti, wafanyakazi wao, maafisa na yeyote anayetekeleza wajibu wa serikali hiyo, wamekiuka sheria.Wanataka mahakama itamke kuwa ushuru uliowekwa kwa sasa, ni mkubwa sana na unapaswa kuangaliwa upya.

Katika hati ya kiapo iliyoamabatanishwa na malalamishi hayo, ambayo yaliandikwa na Bw Maina ambaye ni mwenyekiti wa MSMAE, ni ombi la umma ruzuku ya ada hiyo ikubaliwe ili izuie ukiukaji wa haki na sheria.

“Bunge la kaunti katika mchakato wake wa kuandaa sera hiyo, haikuzingatia maoni ya washikadau wa biashara hiyo au jamii ya wanabiashara,” Bw Maina alisema katika hati hiyo ya kiapo.

Isitoshe wanataka amri itolewe ya kuzuia serikali ya kaunti kuingilia ada ya sasa iliyoko kwa waendesha biashara ya muguka ambayo kwa sasa ni Sh50,000 hadi Sh80,000.

Pia walitaka serikali ya kaunti izuie kuhitilifaiana na biashara yao wakati ambapo kesi hiyo inasubiriwa kusikizwa na kuamuliwa.

You can share this post!

Asukumwa jela miaka 5 kwa kumrusha mwanadada kutoka orofa...

TAHARIRI: Muda mfupi wa kulipa Hustler Fund hakika haufai

T L