Habari Mseto

Wauzaji vitabu walia wanapata hasara

September 3rd, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

WAMILIKI wa maduka ya vitabu mjini Mombasa wameitaka serikali iwaepushie hasara inayotokana na kubadilishwa kwa vitabu hivyo mara kwa mara.

Walisema miaka ya sasa wizara ya elimu imekuwa na mazoea ya kubadilisha vitabu kabla ya shehena ya vitabu waliyonunua kuuza kumalizika madukani mwao.

Bw Abbas Mohammed anayehudumu katika duka la vitabu la Coastal Emporium, alisema mara kwa mara huwa wanasalia na rundo la vitabu visivyokua na umuhimu.

“Tunanunua shehena lakini baada ya kuuza vitabu vichache unasikia kuwa vitabu vipya vimetolewa jambo linalotufanya kuuza vitabu tulivyonavyo kwa bei ya kutupa au kuvipeana bure kwa shule waweke kwa maktaba zao,” akasema.

“Tunashangaa kwa sababu daima moja ukiongeza moja ni mbili hakuna siku itabadilika sasa iweje kila uchao vitabu vipya kutoka kwa watunzi tofauti vinapendekezwa kisha baada ya muda vinatolewa,”alisema.

Kilio chake kiliungwa mkono na Bi Amina Patel anayehudumu katika duka la vitabu la Salmanji, ambaye alieleza kuwa mbeleni hawakuwa na wasiwasi shehena ya vitabu viliposalia kwa sababu walijua wataviuza mwaka unaofuata.

“Sielewi kama kinachoangaliwa ni ubora wa kitabu au tu kufanya biashara,” alisema.

Bi Patel alieleza kufuatia hali hiyo wamiliki wengi wa maduka ya vitabu wamelazimika kupunguza shehena wanayochukuwa na wengine wamelazimika kufunga biashara zao kwa sababu ya kupata hasara.

Bi Halima Imran, ambaye ni mzazi wa mwanafunzi wa darasa la saba, alisema mabadiliko hayo yanamuathiri zaidi mzazi ambaye ana watoto kadha.

Alieleza kuwa wakati wake mzazi alikuwa akinunua kitabu kisha watoto kupokezana jambo lililomfanya kutumia kiasi kidogo cha fedha, ikilinganishwa na sasa ambapo mzazi analazimika kununua vitabu vipya kwa kila mtoto.

“Tulikuwa tunanunuliwa vitabu kisha kila tukienda darasa la mbele unamuachia mdogo wako kitabu hicho lakini sasa jambo hilo haliwezekani,”aliongeza.