Wauzaji walalama kwa kukosa biashara kongamano la Kisumu

Wauzaji walalama kwa kukosa biashara kongamano la Kisumu

NA KENYA NEWS AGENCY

WAFANYABIASHARA katika Kaunti ya Kisumu wanalalamikia kutonufaika kimapato wakati wa Kongamano la Majiji Afrika, lililokamilika majuzi jijini Kisumu.

Wafanyabiashara wengi walikuwa wameweka bidhaa zao katika fuo za Dunga na Hippopoint.

“Tulichukua hata mikopo ili kuongeza bidhaa zetu kutokana na idadi kubwa ya wageni tuliyotarajia. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha wamepata kila kitu walichohitaji. Hata hivyo, tunakadiria hasara baada ya samaki ambao baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wamenunua kuharibika. Imetulazimu kuwatupa,” akasema, Bi Beatrice Okello, ambaye ni mfanyabiashara.

Wafanyabiashara hao ambao walisema kuwa hawakufaulu kutimiza malengo yao, walieleza kuwahali hiyo, inaashiria kuwa kongamano hilo halikutangazwa vizuri ili kuwavutia watu zaidi.

“Tulikuwa na matumaini mengi. Tulinunua vyakula vingi, baadhi yavyo vikiwemo samaki. Tulitarajia uwepo wa wageni wengi lakini kongamano hilo lilivunja matarajio yetu,” akalalama Bi Verol Anyango, ambaye pia ni mfanyabiashara.

Wafanyabiashara hao pia wamelalamika kuwa kongamano limewaachia mzigo wa kulipa mikopo hata bila ya kupata faida yoyote.

“Tulikuwa tumejitayarisha vilivyo kwa kongamano hili. Hata hivyo, tumesikitishwa sana na matokeo yake. Ikiwa kutakuwa na makongamano mengine, tunaomba yawahusishe wenyeji kwenye taratibu za maandalizi yake,” mfanyabiashara mwingine alieleza.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wapinga likizo ya katikati ya muhula

Wito serikali ifanye kila iwezalo uchaguzi usiyumbishe...

T L