Wauzaji watoroka ada nyingi za kaunti

Wauzaji watoroka ada nyingi za kaunti

Na STEPHEN ODUOR

BIASHARA zaidi ya 50 mjini Tana River zimefungwa huku nyingine kadhaa zikielekea kufungwa kutokana na gharama kubwa ya kuendesha biashara.

Wafanyabiashara wanahamia kaunti za Garissa na Kilifi kufungua ukurasa mpya wakilalamikia kodi ya juu inayotozwa na serikali ya Tana River.

Kulingana nao, usimamizi wa kaunti umefanya iwe vigumu kwa biashara kustawi kufuatia walichotaja kama kuongeza kodi bila kujali.

Mkurugenzi wa Mapato Kase Daido, hata hivyo alieleza kuwa kodi zinazotozwa katika Kaunti ya Tana River ni bora zaidi ya ada zinazotozwa katika kaunti nyinginezo.

Kulingana na Bw Daido, Kaunti ya Tana River imekuwa ikikusanya kiwango cha chini cha ushuru kuliko inavyostahili hivyo basi, pana haja ya kubadilisha hali hiyo.

Alisema wafanyabiashara wanapaswa kulaumiwa kwa masaibu yao kwa sababu hawakujitokeza katika warsha za kushirikisha umma walizoalikwa.

“Mabadiliko ya utamaduni daima hukumbwa na upinzani lakini watu watazoea baada ya muda, tunachofanya ni kwa maslahi ya kila mmoja kwa jumla,” alisema.

Mkurugenzi huyo vilevile aliwahimiza wafanyabiashara kutathmini tena soko katika kaunti hiyo kabla ya kuhama.

Bi Janet Musyimi, ambaye amekuwa muuzaji nguo mjini Hola kwa miaka saba iliyopita, alieleza Taifa Leo kuwa, kuongezwa ghafla kwa ada za leseni hakuambatani na mapato yake ndiposa anahitaji kutafuta mazingira bora kwa bidhaa zake.

“Imekuwa vigumu mno kwangu kustahimili, ukuaji umekwama kwa kuwa mapato yote yanatumika kulipia kodi ya duka na ada chungu nzima zinazotozwa,” alisema.

Kulingana na Bi Musyimi, usimamizi wa kaunti haukufanya utafiti wa soko kabla ya kuongeza na kutoza kodi lakini badala yake, uliiga kodi kutoka kaunti nyinginezo za mashinani.

Wafanyabiashara hao walieleza kuwa, kinyume na miaka mitano iliyopita, biashara katika kaunti hiyo imeshuka mno hivyo kusababisha matokeo duni na mkondo mbaya kutokana na janga la Corona.

You can share this post!

Viwanda kununua maziwa kuanzia Sh33

Aliyekuwa msimamizi wa ikulu aombolezwa