Wavamiwa na nyuki baada ya kuiba mtungi wa gesi na televisheni

Wavamiwa na nyuki baada ya kuiba mtungi wa gesi na televisheni

Na SAMMY WAWERU

WANAUME wawili mtaa wa Langas, Eldoret wamelazimika kurejesha mtungi wa gesi na televisheni waliyoiba baada ya kuvamiwa na nyuki. 

Kwenye video na picha zilizosambaa mitandaoni wikendi, mwanamume mmoja alionekana mkono wake wa kulia umevamiwa na bumba la nyuki.

Wa pili naye, alionekana amewekelea mtungi wa gesi kichwani, wakisindikizwa na umma kuelekea katika kituo cha polisi, baada ya kujisalimisha.

“Tulifungua nyumba kwa ufunguo tuliokuwa nao tukachukua mtungi wa gesi na televisheni,” mmoja wao akaambia maafisa wa polisi, wakati wakihojiwa kituoni mbele ya wanahabari.

Inasemekana waliokolewa na maafisa wa polisi, ambapo umma ulikuwa umetishia kuwaangamiza. Duru zinaarifu walichukua hatua hiyo baada ya mmiliki kuwaendea kwa mganga.

Kufuatia tukio hilo, wachangiaji katika mitandao walizua ucheshi wakitaka kuelekezwa kwa mganga aliyedaiwa kuwashinikiza kurejesha vifaa hivyo.

“Naomba nambari za rununu za mwenye kuwatumia nyuki, tafadhali,” #Christina Alexander akasema kwenye Twitter.

“Huyo mganga yuko sawa, leteni nambari zake za simu,” akachangia Eussy Euslah.

You can share this post!

Kenya kunufaika na kuchaguliwa kwa Maluki kuwa mwenyekiti...

Wachuuzi 500 wakosa pa kuuzia baada ya vibanda kubomolewa...