Habari Mseto

Wavinya alaani hatua ya kanjo kukazia madiwani maisha

February 1st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

GAVANA wa Machakos Wavinya Ndeti ameamuru uchunguzi wa haraka kufanywa kufuatia madai kuwa maafisa wa idara ya ulinzi almaarufu kanjo katika kaunti hiyo, huwadhulumu madiwani.

Kauli yake inajiri baada ya kisa cha Jumatano ambapo diwani wa wadi ya Kalama Boniface Maeke alitendewa unyama na maafisa wa kanjo.

Bi Ndeti alitoa makataa ya siku saba kwa Katibu wa Kaunti na Mkuu wa Utumishi wa Umma kumkabidhi ripoti ya uchunguzi.

“Ninataka ripoti hiyo iwasilishwe afisini mwangu siku saba baada ya leo (Januari 31, 2024). Baadaye nitachukua hatua kali dhidi ya wahusika wote,” akasema Bi Ndeti bila kutaja jina la diwani aliyedhulumiwa na maafisa wake nje ya majengo ya mahakama.

Alisikitika kabisa kwa kile kilichotendeka na kutoa hakikisho kuwa serikali yake haitavumilia visa vya uvunjaji wa sheria vinavyoendelezwa maafisa wa kaunti dhidi ya raia na viongozi.

Aidha, gavana huyo alitoa wito kwa maafisa wote wa idara ya ulinzi katika kaunti hiyo kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu za kazi wanapoendesha majukumu yao nyakati zote.

“Vile vile, wanafaa kuheshimu haki za wakazi wote wa Machakos nyakati zote jinsi ambavyo imekuwa kawaida yetu,” Gavana Ndeti akaongeza.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kaunti ya Machakos Anne Kiusya alilaani kisa hicho na kuwataka maafisa wa polisi kufanya uchunguzi kwa lengo la kuwaadhibu wahusika.

“Tunaamini kwamba polisi watachukua hatua na kuwahakikishia madiwani wetu usalama pamoja na raia wa kawaida ili kuzuia vitendo aina hii vya kikatili siku zijazo,” akasema.

Baada ya kisa cha Jumatano, ambapo Bw Maeke alidhulumiwa na maafisa wa kaunti ya Machakos walipojaribu kumkamata, kiongozi huyo aliwaambia wanahabari kwamba alivuliwa nguo na maafisa hao.

“Sijui ni kwa nini walinivamia. Ninawafahamu vizuri, wanafanya kazi katika Serikali ya Kaunti ya Machakos kama maafisa wa ulinzi,” Bw Maeke akaeleza.

Alisema kuwa alikuwa ameandamana na mwenzake, diwani wa wadi ya Masii/Vyulya Douglas Musyoka mahakamani aliposhambuliwa na maafisa hao.

Maafisa hao walikuwa wamemkamata Bw Musyoka Jumanne kwa kosa la kujenga nyumba bila idhini kutoka kwa idara husika katika Kaunti ya Machakos.

Diwani huyo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu.

Diwani Maeke alijeruhiwa mikononi na miguuni wakati wa kisa hicho na kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Machakos.