Kimataifa

Wavumbuzi wa Instagram wajiuzulu ili wapumzike

September 25th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

WAVUMBUZI wa mtandao wa kijamii wa kuchapisha picha Instagram Kevin Systrom na Mike Krieger walijiuzuli kama Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) na Afisa Mkuu wa Kiufundi na teknolojia.

Kampuni ya apu hiyo ya picha ilitangaza haya Jumatatu jioni, japo wawili hao hawakueleza kiini hasa cha wao kuondoka.

Systrom alisema kupitia mtandao mmoja kuwa waliamua kupumzika kidogo na kuzuru “kutaka kujua na ubunifu tena.”

Kulingana na shirika la Instagram, ambalo lilinunuliwa na kampuni ya Facebook kwa dola1 bilioni mnamo 2012, haifahamiki siku yao ya mwisho kufanya kazi itakuwa lini, lakini ishara zinadokeza kuwa hawatakaa sana.

Jumatatu walifahamisha Instagram na Facebook kuhusu wazo lao la kujiuzulu, kulingana na Instagram.

Instagram ina zaidi ya watumizi bilioni moja wa kila mwezi kila wakati na imekua zaidi baada ya kuongeza vigezo kama watu kuchapisha jumbe na video fupi.

Instagram sasa ndio ndilo tawi la Facebook ambalo linakua kwa kasi zaidi na kuleta mapato mengi. Kuondoka kwa waanzilishi hao wa mtandao wa Instagram sasa kumekuja miezi michache baada ya mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Whatsapp Jan Koum, ambao pia ni tawi la Facebook kujiondoa.

“Kuzindua vitu vipya kunatuhitaji kuondoka kwanza, kuelewa kile kinachotupa motisha na kulainisha hicho na mahitaji ya dunia, hicho ndicho tunalenga kufanya,” akasema Systrom.

Walisema wana maono mema kuwa Instagram na Facebook zitazidi kukua siku zijazo.

CEO wa Facebook Mark Zuckeberg aliwataja Systrom na Krieger kuwa “viongozi wasio wa kawaida wa bidhaa.”

“Naatazamia kuona kile watakachobuni kutoka sasa,” akasema Zuckerberg kwa ujumbe aliotuma.