Habari za Kaunti

Wavunaji mchanga wachapa kazi licha ya kufukua mafuvu

January 31st, 2024 2 min read

NA KASSIM ADINASI

UVUNAJI wa mchanga kwenye maeneo mengi ya Usonga katika Kaunti ya Siaya unakuja na makubwa yake, la hivi punde likiwa ni wavunaji kukumbana na mafuvu ya watu waliozikwa zamani.

Pia wakazi wengi waliozungumza na Taifa Leo walisema uvunaji wa mchanga kwa kiwango kilichopitiliza kumesambaratisha uchukuzi na usafiri katika maeneo hayo.

Wakazi wa maeneo hayo kwa ujumla wameanza kuzoea kukutana na mafuvu na mifupa ambayo hufukuliwa wakati wa uvunaji wa mchanga.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Sidundo, Milambo, na Udamai ambako hakuna barabara za kisasa.

Bw Nicolas Agwanda kutoka Milambo anasema shughuli za uvunaji wa mchanga zimeharibu kijiji chao.

“Mabonde makubwa na mashimo makubwa yamefanya vigumu magari kupita,” akasema Bw Agwanda.

Ingawa ujasiri wa wavunaji mchanga huo hutokana na ari ya kutafutia familia zao, umeharibu mazingira pakubwa.

Bw Agwanda anasema juhudi za wanakijiji kuripoti suala hilo kwa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) hazijazaa matunda.

Kwa kushirikiana na naadhi ya wanakijiji, wavunaji wa mchanga wameharibu makaburi na hata barabara.

Barabara mbovu Usonga, Kaunti ya Siaya. PICHA | KASSIM ADINASI

Naye Bw Bonface Agoro wa kutoka Sidundo ana hofu kwamba shughuli hizo zinavunja turathi za jamii kwa sababu zinaharibiwa pakubwa.

“Wanapovuna mchanga, wanatupa baadhi ya rasilimali muhimu ambazo ziliachwa na wavyele wetu,” akalalamika Bw Agoro.

Anaongeza kwamba hali iliyoko kwa sasa ni hatari mno wakati wa dharura.

“Tukiwa na mgonjwa, tunalazimika kumbeba mgongoni kwa sababu barabara hazipitiki kutokana na mashimo makubwa yaliyoachwa. Baya zaidi ni kwamba ni tunabeba hata majeneza ya maiti kwa mwendo mrefu tukienda kuzika wapendwa wetu,” akasema.

Mkazi mwingine, Bw Charles Oloo anasema malori makubwa yanayofika vijijini kubeba mchanga yanaharibu mahandaki ya kupitisha majitaka.

“Malori yakiharibu mahandaki tunabaki na mfumo duni wa kupitisha maji hivyo mvua ikinyesha kunakuwa na matope na mafuriko,” akasema Bw Oloo.

Pia anasema sasa wakazi wametishia kuchukua hatua mkononi.

“Tukifikia hatua ya kuchukua sheria mkononi, yeyote asitulaumu,” akaongeza.

Anasema wakazi wamechoshwa na hali hiyo.

[email protected]