Habari Mseto

Wavuvi 24 wa Kenya wabambwa na polisi UG

May 23rd, 2019 1 min read

Na George Odiwuor

WAVUVI 24 kutoka Kenya wanazuiliwa nchini Uganda baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka sheria za uvuvi wakiendesha shughuli zao katika Ziwa Victoria Jumatano usiku.

Wavuvi hao walikamatwa na maafisa wa usalama kutoka Uganda ambao walikuwa wakiendesha doria katika ziwa hilo.

Maafisa hao kutoka Kisiwa cha Homa nchini Uganda pia walitwaa vifaa vya uvuvi vya Wakenya hao (vikiwemo nyavu na boti nane).

Wale waliokamatwa wanatoka maeneobunge ya Suba Kaskazini na Suba Kusini, katika Kaunti ya Homa Bay.

Walidaiwa kuwakamata wavuvi 21 kutoka fuo za Sare na Nyandiwa katika eneo bunge la Suba Kusini kabla ya kuwakamata wengine watatu katika Kisiwa cha Remba kilichoko eneo bunge la Suba Kaskazini.

Wavuvi kutoka Sare na Nyandiwa walikuwa wakiendesha maboti saa ilhali wale kutoka Remba walikuwa wakihudumu katika boti moja.

Mwenyekiti wa Shirika la Usimamizi wa Fuo katika Kaunti ya Homa Bay Edward Oremo alisema thamani ya vifaa vya uvuvi ambavyo vinazuiliwa nchini Uganda haijulikani.