Wavuvi Kilifi watakiwa wawe waangalifu upepo mkali ukivuma baharini

Wavuvi Kilifi watakiwa wawe waangalifu upepo mkali ukivuma baharini

NA ALEX KALAMA 

WAVUVI na watu wanaofanya kazi katika fuo za bahari katika Kaunti ya Kilifi wametakiwa kuwa makini wanapofanya shughuli zao baharini.

Kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa msimu huu kunashuhudiwa ongezeko la upepo na mawimbi makali baharini na hali hiyo huenda ikahatarisha maisha ya watu iwapo tahadhari haitachukuliwa.

Aidha Idara hiyo imeeleza kuwa hali ya ukame itaendelea kushuhudiwa kwa kipindi kirefu hadi mwezi wa tatu au wa nne kabla ya kipindi cha mvua nyingi kuanza kushuhudiwa.

Wavuvi wakijipanga kuendelea na shughuli zao katika Bahari Hindi, Kaunti ya Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Akizungumza na Taifa Leo mjini Kilifi, Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa katika Kaunti ya Kilifi Geofrey Ogutu ameeleza kuwa vipindi vya joto vinatarajiwa kupanda nyakati za mchana huku vipindi vya joto nyakati za usiku vikikadiriwa kuwa kati ya nyuzi 23 hadi 26.

“Hali ya kiangazi bado itaendelea kwa muda hapa Kilifi kwa sababu ile mvua tunapata kidogo ni ile ambayo iko nje ya msimu, na msimu mwingine wa mvua tunatarajia kuanzia Machi, Aprili na Mei. Kwa sasa hatujatoa utabiri bado wa huo msimu. Utabiri kuhusu huo msimu wa mvua utatoka mwishoni mwa mwezi wa Februari. Tuko kipindi kigumu mpaka huo msimu mwingine uanze,” akasema Bw Ogutu.

Fauka ya hayo Ogutu aliwashauri wakulima katika Kaunti ya Kilifi kufuatilia utabiri wa msimu wa mvua ndefu zinazotarajiwa kati ya mwezi Machi hadi mwezi Mei ambao unatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi Februari ili kuanza kutayarisha mashamba kwa ajili ya upanzi.

Wavuvi wakijipanga kuendelea na shughuli zao katika Bahari Hindi, Kaunti ya Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

“Kwa wale wanaofanya biashara au shughuli kwa bahari wafahamu tuko kwa ule msimu ambapo upepo unaenda juu zaidi na mawimbi yanakuwa na nguvu nyingi mno. Wafuatilie kwa karibu utabiri wa hali ya bahari vile tunapeana kila wiki. Na pia ikiwa wewe ni mkulima kuna umuhimu wa kufuatilia kwa makini utabiri wa msimu wa mvua ili ujue ni wakati gani unafaa kutayarisha shamba kabla msimu wa mvua kuanza,” amesema Bw Ogutu.

Upepo mkali husababisha hasara baharini na katika fuo za bahari. PICHA | MAUREEN ONGALA
  • Tags

You can share this post!

Raha ya wadau meli ya watalii 620 ikitia nanga

Kiongozi wa IS auawa nchini Somalia

T L