Habari Mseto

Wavuvi wavua mabomu 3 badala ya samaki

April 23rd, 2019 1 min read

Na GEORGE ODIWUOR

HALI ya taharuki imekumba wakazi katika ufukwe wa Kiumba, Kisiwani Rusinga, Homa Bay baada ya wavuvi kunasa mabomu matatu yanayosadikiwa kuachwa na wakoloni katika nyavu zao.

Wavuvi hao walikuwa wakivua samaki ndani ya Ziwa Victoria kama ilivyo kawaida yao. Badala yake, nyavu zao zilinasa mabomu.

Mabomu hayo yaliyochakaa kwa kutu, yanaaminika kutupwa ndani ya Ziwa Victoria na wakoloni wakati wa vita.

Mabomu hayo yalikuwa ndani ya kijisanduku kilichotengenezwa kwa mbao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Ufuo (BMU) ya Kiumba, Samuel Odira alisema wavuvi hao waliwafahamisha maafisa wa usalama ambao waliwasili na kubeba mabomu hayo hadi ufuoni.

Afisa Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Jinai (DCI) wa Homa Bay, Daniel Wachira alisema amewasiliana na wataalamu wa kutegua mabomu kutoka Kisumu ambao wanatarajiwa kukagua kwa makini silaha hizo. Wataalamu hao watachunguza ikiwa mabomu hayo yangali na uwezo wa kulipuka.