Habari Mseto

Wawakilishi Wanawake hawana manufaa, wabunge wapunguzwe hadi 47 – Kabogo

September 27th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu William Kabogo amejiunga na mjadala wa viongozi wanaopigania kubadilishwa kwa katiba ili kuondoa baadhi ya viti vya uwakilishi wa wananchi, akishikilia kuwa viti vya Wawakilishi Wanawake haswa vinafaa kuondolewa kabisa.

Bw Kabogo amesema kuwa wawakilishi wanawake hawana manufaa yoyote, akisema sheria ya thuluthi mbili katika uwakilishi wa jinsia haifai kutumika kwenye uchaguzi, kwani kulingana naye huko ni kulazimishia wananchi viongozi.

Akizungumza katika Runinga ya Citizen Jumatano usiku, Bw Kabogo aidha alitaka idadi ya wabunge kupunguzwa kutoka 290 hadi 47 ili kuwiana na idadi ya kaunti, huku ya wawakilishi wadi akitaka ifike 290 kama idadi ya maeneobunge.

“Hii hadithi ya uwakilishi wa jinsia na sheria ya thuluthi mbili tuisahau katika uchaguzi, ikiwa mwanamke anataka uongozi aende debeni si kutenga nafasi fulani kuwa za wanawake. Tunahitaji kuwakilishwa na maseneta 47, wabunge 47 na magavana 47, hiyo inatosha,” akasema Bw Kabogo.

Bw Kabogo alisema hali hii itasaidia ili wakati sheria za kutoza wananchi ushuru zinapotaka kubadilishwa, viongozi waliochaguliwa watetee ipasavyo.

“Watakaochaguliwa watawakilisha wote wanaume na wanawake kama inavyofanyika duniani kote, si kuanza kutengea wanawake viti fulani na kuwalipa tu,” akasema gavana huyo wa zamani.

Aidha, kulingana na Bw Kabogo, idadi ya madiwani inafaa kuwiana na ile ya maeneobunge ili kupunguza mzigo wa mishahara na matumizi mengine ya serikali.

Kiongozi huyo sasa amejiunga na wengine ambao wamekuwa wakipigania kubadilishwa kwa katiba na kuondolewa kwa viti vya wawakilishi wa kina mama.

Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Uasin Gishu Gladys Boss Shollei aidha mbeleni alipendekeza viti hivyo kuondolewa, akisema wanawake wanafaa kumenyana na wanaume uchaguzini badala ya kupewa nafasi ya bure.