Wawaniaji 16 wa urais wawasilisha saini zao kwa IEBC

Wawaniaji 16 wa urais wawasilisha saini zao kwa IEBC

NA JURGEN NAMBEKA

ANGALAU wagombeaji 16 wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, waliwasilisha sahihi pamoja na nakala za vitambulisho, kama walivyotakiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC), kufikia Mei 25.

Kati ya waliofaulu kuwasilisha stakabadhi kwa IEBC, 10 ni wagombeaji wa vyama vya kisiasa hali waliosalia ni wagombeaji huru.

Miongoni mwa wagombea hao wa urais katika uchaguzi wa Agosti 9, wanaosimama kupitia vyama vya kisiasa ni kinara wa ODM Bw Raila Odinga, Naibu wa Rais Dkt William Ruto, Kalonzo Musyoka, Jimi Wanjigi, Austine Njeri Gathangu, Prof George Wajackoyah, Walter Mong’are, Mwaure Waihiga, Mwangi wa Iria, na Justus Juma.

Wagombea huru waliowasilisha majina yao ni Dorothy Kemunto, Faith Wairimu Ngigi, Grita Muthoni, Reuben Kigame, Gibson Ng’anga na Jeremiah Nyaga.

Bw Odinga anayewania urais kwa mara ya tano atapeperusha bendera ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, huku Dkt Ruto akiwania kupitia chama cha UDA, kinachohusishwa na muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Musyoka ambaye awali alikuwa katika muungano wa Azimio kabla ya kutishia kugura kwa kutopewa nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga, ananuia kuwania kupitia chama cha Wiper.

Mfanyabiashara Wanjigi ambaye hapo awali alikuwa rafiki wa karibu wa Bw Odinga, anawania kiti cha urais kupitia chama cha Safina cha wakili Paul Muite.

Bw Mwangi wa Iria atatumia chama cha Usawa kwa Wote kugombea kiti hicho huku mwenzake Prof Wajackoya akiwania kupitia chama cha Roots Party.

Bw Wa Iria na Prof Wajackoyah wamekuwa katika vinywa vya Wakenya baada ya kutoa ahadi ya ng’ombe wa maziwa kwa kila boma na kupanda na kutumia bangi kukomboa uchumi wa nchi mtawalia.

Bw Mong’are aliyepata umaarufu humu nchini kama mchekeshaji stadi kwa kumuiga Rais Mstaafu Daniel arap Moi, atawania kupitia chama cha Umoja Summit Party.

Wakili wa mahakama ya juu Bw Mwaure aliyewasilisha stakabadhi zake kwa wakati ufaao, atawania kupitia chama cha Agano.

Mabw Juma na Kathangu, wanasaka kiti cha urais kupitia vyama vya Justice and Freedom na Ford Asili mtawalia.

Hapo awali, wagombeaji huru walilamikia mahitaji kadhaa ya IEBC hasa lile la kukusanya nakala za vitambulisho.

Licha ya hayo, msanii wa nyimbo za injili Bw Kigame na wagombea huru wengine, walijitahidi ili wasitupwe nje ya kinyang’anyiro.

IEBC sasa ina siku tano kupitia saini na nakala za vitambulisho vilivyowasilishwa na wagombea hao.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati alieleza kuwa watapitia nakala hizo kubaini iwapo saini zilizokusanywa ni halali.

Dkt Ekuru Aukot wa Third Way Alliance pamoja na Dkt Japheth Kaluyu waliowania urais mnamo 2017, ni miongoni mwa wawaniaji walioshindwa kuwasilisha nakala za saini kwa wakati ufaao.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi waulizia aliko gavana wao

Equity kutoa huduma kupitia WhatsApp, Facebook, Telegram

T L