Habari

Wawekezaji sekta ya utalii wadai wito wa Balala hauna mashiko

July 27th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WAMILIKI wa hoteli za ufuoni wamemshtumu Waziri wa Utalii Bw Najib Balala kwa kuwataka wapunguze ada wanazotoza ili kuvutia watalii wa humu nchini.

Aidha Bw Balala alilalamika kuhusu gharama ya utalii akisisitiza kwamba endapo wanataka kuwavutia watalii wa humu nchini, ni sharti wapunguze ada katika sekta hiyo.

Waziri huyo alisema Wakenya wengi hawazuru sehemu nyinginezo za humu nchini kwa sababu ya gharama za hoteli ambazo alizitaja kuwa ghali mno.

“Tumezoea au kuharibiwa na soko la kimataifa kwa kuwatoza watalii bei yakimataifa. Tuna vituo bora zaidi za utalii lakini hatuwezi kutoza bei ya juu, hili ndilo swala nyeti kwenye sekta hii na ninashida kubwa na sekta hii,” alisema waziri huyo kwenye mahojiano hivi majuzi huku akiwataka wakenya kuwa katika mstari wa mbele kuinua sekta ya utalii kwa kuzuru sehemu za utalii.

Waziri huyo alisema wakenya wengi wataamua kwenda mashambani mwao kujiunga na familia zao badala ya kuzuru sehemu za utalii kutokana na gharama ya juu wanayotozwa.Alisema gharama ya juu ni changamoto kubwa kwenye sekta ya utalii.

Bw Balala aliwasihi watalii wa humu nchini kuwa katika mstari wa mbele kutembelea “maeneo yetu ya utalii” na kuinua sekkta hiyo ambayo imefifia kutokana na janga la corona.

Hata hivyo, wamiliki wa hoteli wamemtaka waziri huyo kuhaskikisha serikali inapunguza ada mbali mbali wanazotozwa.

Walitaja gharama za stima, maji na ushuru kugharimu faida wanazopata kwenye sekta hiyo.

“Sekta yetu inatumia fedha nyingi sana hususan katika uajiri wa wafanyikazi. Serikali inafaa kufahamu umuhimu wa utalii na kuwekeza kwenye sekta hii ambayo imekuwa muhimu kwa uchumi wetu. Kwa mfano, serikali inafaa kuondoa ada au kupunguza ushuru mwingi tunaotozwa. Ili kuokoa sekta hii ambayo inasaidia wengi wakiwemo wakulima, serikali inafaa kutuokoa,” alisema afisa mkuu wa muungano wa wahudumu wa hoteli nchini Dkt Sam Ikwaye.

Dkt Ikwaye alitetea ada za juu zinazotozwa kwenye hoteli akisisitiza Wakenya wana uwezo wa kuchagua hoteli wanazopaswa kuzuru kulingana na uwezo.

“Tuna aina nyingi za hoteli zinazotoza bei tofauti, soko ni kubwa sana. Lakini waziri anafaa kujua hatuwezi kupunguza ada kama kweli ana nia ya kuokoa sekta hii afanye mikutano na wawekezaji ili kutafuta suluhu,” alisema mtaalam huyo wa utalii.

Alitoa mfano wa nchi za utalii kama Misri na Malaysia ambapo serikali zao zimegharimia ada nyingi kufanya sekta ya utalii kuimarika.