Habari za Kitaifa

Wawekezaji wa kibinafsi walionyakua ardhi ya umma waonywa

January 20th, 2024 1 min read

NA BARNABAS BII

HUENDA mamia ya watu wakafurushwa makwao huku serikali ikilenga kutwaa ardhi ya umma iliyonyakuliwa kote nchini.

Hii inalenga kuwezesha utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Rais William Ruto ametoa notisi kwa wawekezaji wa kibinafsi ambao wamenyakua ardhi ya umma kinyume cha sheria kuzisalimisha au wafurushwe kwa nguvu ili kuwezesha utekelezaji wa ajenda yake ya maendeleo katika ujenzi wa makazi, kilimo, ujenzi wa viwanda miongoni mwa mipango mingine.

Amewaagiza maafisa wa Wizara ya Ardhi na wasimamizi wa kitaifa na kaunti kuratibu urejeshaji wa mashamba ya umma yaliyonyakuliwa akibainisha kuwa kunapunguza kasi ya kuanzishwa kwa miradi muhimu ya maendeleo nchini kote.

“Wanyakuzi hao wa ardhi wana chaguo moja pekee, ambalo ni kusalimisha ardhi ya umma na kuhama kabla hatujachukua hatua,” alisema Dkt Ruto mara kwa mara alipozuru baadhi ya kaunti za Bonde la Ufa kuzindua miradi ya nyumba za bei nafuu.