Makala

WAWERU: Aibu mabilioni kuporwa huku kukishuhudiwa uhaba mkubwa wa chakula

September 11th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa miezi miwili iliyopita baadhi ya maeneo nchini hasa yanayoshuhudia kiangazi mara kwa mara yameripotiwa kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula njaa.

Kaunti zilizotajwa kuathirika pakubwa ni Wajir, Marsabit, Laikipia, Isiolo, Tharaka Nithi na Baringo, miongoni mwa nyinginezo.

Tayari asasi za habari zimetua humo na kufichua masaibu wanayopitia waathiriwa. Hii ni licha ya serikali kudai hali si kama inavyoripotiwa.

Mapema 2019 watu kadhaa Kaunti ya Baringo waliripotiwa kufa njaa. Hata hivyo, serikali ilikanusha kutokea maafa hayo ikidai yalisababishwa na magonjwa.

Kitengo cha majanga ya kitaifa, NDMU, kwa kawaida hutoa tahadhari kwa serikali na tayari kimepuliza kipenga.

Wasamaria kwa ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu, wameonekana kuachiwa wajibu kushughulikia raia wanaohangaishwa na njaa.

Imekuwa mazoea kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua maafa yanapotendeka. Pandashuka wanazopitia wahanga wa njaa zinashuhudiwa mabilioni ya pesa yakiishia kwenye mifuko ya wachache, wenye tamaa ya ubinafsi kupitia ufisadi.

Mwaka huu pekee, sakata za mabilioni ya pesa kufujwa katika wizara kadhaa na taasisi mbalimbali za serikali na vilevile katika serikali za kaunti, zimeripotiwa.

Ni aibu Wakenya – tena wanaolipa ushuru – kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula huku fedha zinazopaswa kuwahudumia zikipondwa na wachache walafi.

“Ushuru tunaolipa unatosha kukithi mahitaji ya kila Mkenya. Hii ni nchi yenye ukwasi mkubwa na unaoweza kuiendelea kimaendeleo bila kutegemea mikopo na misaada ya kigeni,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi Michael Muriuki.

Kulingana na mtaalamu huyu mianya inakopotelea mali ya umma ndiko shida zimetoka. Akitumia mgao unaopokewa na serikali za kaunti kutoka kwa Hazina ya Kitaifa, Bw Muriuki anasema magavana wanapaswa kuelekeza kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo.

“Ninashangaa kuona wakidai mgao zaidi ilhali pesa wanazopokea nyingi yazo inaelekea kulipa wafanyakazi. Kwa nini wasipunguzwe, watilie maanani maslahi ya Wakenya?” ahoji.

Ikizingatiwa kuwa sekta ya kilimo imegatuliwa kupitia katiba ya sasa na iliyozinduliwa 2010, Bw Muriuki anahoji huenda ndiyo sababu serikali kuu inajikokota kushughulikia masaibu ya njaa.

“Serikali ya kitaifa imetua mzigo huo kwa magavana, ambao wanapaswa kuboresha maeneo yao,” anaeleza.

Hata hivyo, mtaalamu huyu anasema Matunda ya ugatuzi na yanayopaniwa kumuwezesha kila Mkenya kupata huduma za serikali yataonekana suala la ufisadi likiangamizwa.

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza vita kali dhidi ya ufisadi, akishinikiza taasisi husika kama ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP, upelelezi wa jinai DCI na tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kutosaza yeyote anayepora na kufuja mali ya umma.

Wataalamu wa kilimo kwa upande wao wanasema mashamba ya Kenya yakitumiwa ipasavyo suala la njaa litazikwa katika kaburi la sahau.

“Majirani wetu kama vile Tanzania na Uganda, kilimo kimetiliwa maanani. Mashamba yanatumiwa ipasavyo, serikali ikipiga jeki raia wake kwa pembejeo; mbegu na mbolea,” anasema mtaalamu Nicholas Njoroge.

Anaendelea kueleza kwamba fedha zinazopondwa na viongozi wenye tamaa na ubinafsi zikielekezwa katika uchimbaji wa mabwawa na uvunaji wa maji msimu wa mvua, baa la njaa linaloshuhudiwa litakuwa likisomwa kwenye vitabu na magazeti “Kenya wakati mmoja ilionja makali ya njaa lakini kupitia mikakati kabambe iliangaziwa kikamilifu”.

“Wakulima waliokumbatia mfumo wa uvunaji maji nchini na kuzalisha mazao ni kielelezo kwa serikali. Mataifa kama Misri na Israili ni janga, lakini tu tunayategemea kwa matunda na mazao mengine,” anasema Bw Njoroge.

Aidha, nchi hizo huwajibikia kila tone la maji ya mvua. Ni muhimu kukumbusha kuwa mataifa yasiyoruhusu ufisadi kusakatwa, njaa kwao ni historia.