Habari Mseto

Wawili kujua hatima yao leo kuhusu mauaji

August 25th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA Chris Philip Obure na mlinzi wake Robert John Ouko Bodo wanaozuiliwa kwa mauaji ya Kelvin Omwenga, watajua hatima yao leo Jumanne.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera, Bw Derrick Kuto, aliamuru kuwa wawili hao wasalie katika kituo cha Polisi cha Kilimani hadi leo Jumanne, atakapoamua ikiwa ataruhusu polisi wawazuilie kwa siku 14 au la.

Kupitia Allan Mogere, afisi ya Mashtaka ya Umma ilitaka siku hizo 14 ili polisi wakamilishe uchunguzi wa kesi, na wapimwe akili kujua utimamu wao kabla ya kushtakiwa kwa mauaji ya Omwenga, aliyekuwa na umri wa miaka 28.

Pia mahakama ilielezwa polisi wanataka kuwahoji na kuandikisha taarifa ya watu wanne waliokuwa na marehemu usiku wa Agosti 22, 2020 katika makazi yake yaliyo katika jengo la Galana lililoko Kilimani, Nairobi.

Bw Kuto alielezwa kuwa polisi wanataka kukagua bastola iliyotumika na pia kukagua picha za CCTV zinazoonyesha Bw Ouko akiingia na kutoka katika makazi ya Omwenga.

Lakini mawakili Profesa PLO Lumumba na Otieno Arum walipinga ombi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao siku 14 wakisema uchunguzi unaofanywa haufai kuchukua siku hizo 14.

Walisema washtakiwa walijisalamisha kwa polisi na wako tayari kushirikiana na polisi kukamilisha uchunguzi.

“Washtakiwa hawatavuruga uchunguzi wa kesi hii na wako tayari kuwasiliana na polisi wanaochunguza kesi hii,” alisema Prof Lumumba.

Hakimu alikuwa na kauli yake.

“Kwa vile mahakama ilianza kusikiza kesi saa saba sina muda wa kutosha kutayarisha uamuzi. Nitautoa kesho (leo) saa nane mchana,” alisema Bw Kuto.