Wawili ndani miaka 30 kwa kuiba teksi kimabavu

Wawili ndani miaka 30 kwa kuiba teksi kimabavu

NA RICHARD MUNGUTI

WANAUME wawili waliomnyang’anya dereva wa teksi gari lake na simu baada ya kumfunga kwa kamba kisha wakamtupa ndani ya mtaro wa majitaka jana Alhamisi walifungwa miaka 30 kila mmoja.

Antony Ekai Mwaiti na Kennedy Karanja Mungai walisukumiwa kifungo hicho na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi aliyewapata na hatia.

Bw Ochoi alisema Mwaiti na Mungai walimfunga kwa kamba dereva huyo wa teksi waliyemkodisha awapeleke katika hoteli ya kifahari ya Ole Sereni, Nairobi.

Pia walimkata vidole kwa kisu alipojaribu kuwazuia kumnyang’anya.

Wawili hao walipatikana na hatia ya kumnyang’anya kimabavu Michael Kanyi gari na simu za thamani ya Sh552,000 mnamo Machi 3, 2016.

Mwaiti na Mungai walimpata Kanyi katika egesho la hoteli ya Hilton na kumsihi awapeleke Ole Sereni.

Kanyi alikubali lakini wakamgeuka katika barabara ya Southern Bypass kwenye mbunga ya Wanyamapori ya Nairobi.

Gari liliisha mafuta na kukwama katika makutano ya barabara ya Muthaiga na Limuru na polisi wakalipata wawili hao wakisubiri bodaboda awaletee mafuta.

  • Tags

You can share this post!

Spika azamisha Azimio bungeni

Njaa yalemea raia msaada wa serikali ukichelewa kufika

T L