Habari Mseto

Wawili waangamia kwa mafuriko Samburu

April 23rd, 2020 1 min read

By GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Watu wawili wamefariki baada ya kusombwa na maji ya mafuriko katika kijiji cha Illaut, katika kaunti ya Samburu.

Wawili hao ni pamoja na mtoto wa miaka sita na mwanamume wa miaka 30.

Afisa mkuu wa programu maalum katika kaunti ya Samburu Daniel Lesaigor alisema kuwa miili ya wawili hao imepatikana baada ya maji kupungua.

“Mafuriko yalitokana na mvua nyingi inayoshuhudiwa. Kijiji kizima kilisombwa na maji ya mafuriko lakini wawili ndio wamethibitishwa kufariki. Wengine wapo salama,” Bw Lesaigor aliambia Taifa Leo.

Idara ya kushughulikia masuala ya dharura kwenye kaunti hiyo ilifanikiwa kuwaokoa makumi ya watu waliozingirwa na maji, kutumia ndege aina ya helikopta.

Bw Lesaigor alisema kuwa mamia ya familia katika eneo hilo lililoko kaskazini mwa kaunti ya Samburu wameachwa bila makao kufuatia mvua kubwa ambayo inaendelea kushuhudia nchini.

“Tunavyozungumza mamia hawana makao kwa sababu nyumba (Manyatta) zao zilisombwa na maji,” alisema.

Alifichua kuwa zaidi ya mifugo mia mbili hamsini iliangamia kwenye tukio hilo. Mbuzi wapatao 250, ngombe watano na idadi ya ngamia isiyojulikana walifagiliwa na maji ya mafuriko.

Kwingineko, watu 11 waliokolewa eneo la Waso baada ya mto Ewaso Nyiro kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa ambayo inaendelea kunyesha.

Lesaigor alisema kuwa waokoaji walitumia ndege ya helikopta kuwaokoa watu hao waliokuwa wamezingirwa na maji.

Alisema watu hao walipatwa na maji kwa ghafla lakini hakuna maafa yaliyoripotiwa.

Alitoa onyo kwa wakazi kuwa macho wanapovuka mito.