Wawili wafariki mamia wakikesha nje baada ya nyumba kuteketea Mukuru

Wawili wafariki mamia wakikesha nje baada ya nyumba kuteketea Mukuru

Na SAMMY KIMATU

WATU wawili wamefariki katika kisa cha moto huku mtu wa tatu akiuguza majeraha katika hospitali nazo familia 131 zikilala nje penye baridi baada ya nyumba zao kuteketea.

Kisa hicho kilitokea mwishoni mwa wiki katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo “A” ulioko wodi ya Nairobi South, kaunti Ndogo ya Starehe.

Tukio hilo limethibitishwa na kinara wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo.

Bw Odingo aliongeza kwamba inadaiwa moto huo ulisababishwa na mashumaa ingawa maafisa wa kampuni ya kusambaza stima nchini (KPLC) wameanzisha uchunguzi wao.

“Ingawa hakukuwa na stima mtaani, KPLC itachunguza zaidi kubaini ikiwa kuna watu waliokuwa wakijiunganishia stima ya wizi wakati wa tukio hilo baada ya trasfoma kuondolewa awali mtaani,” Bw Odingo akasema.

Waliofariki ni mtoto Melvin Anyona, 7 na marehemu Bw James Atambo, 40.

Miili ya wawili hao ilikuwa imeteketea kiasi cha kutotambuliwa kwa urahisi.

Mwenyekiti wa usalama mtaani huo, Bw Moses Mavesi aliambia Taifa Leo kwamba moto ulianza mwendo wa saa sita unusu za usiku.

“Moto ulianzia kwa nyumba ya marehemu Bw Atambo aliyeishi na mwanamume mwenzake aliyeponea kifo kwa tundu la sindano. Marehemu alianguka baada ya moshi kumzindia huku mwili wake ukiteketezwa na ndimi za moto. Mwenzake alifanikiwa kuruka hadi ndani ya mto Ngong na kwa bahati nzuri hakuumia,” Bw Mavesi asema.

Baada ya moto kuzidi na kuenea hadi nyumba jirani, ulipata watoto wawili wakiwa wamelala.

Bw Mavesi alisimulia jinsi kwenye kukurukakara za kujiokoa, msichana wa miaka 13, alianguka kutoka orofa ya kwanza na kuumia mkono wake.

Mwathiriwa, Bw Caleb Njairo, 37, seremala wa Jua Kali aliyeishi mtaani humo kwa muda wa miaka miwili unusu sasa alisema ana machungu ya kumpoteza bintiye kwenye mkasa huo.

“Nilimpenda binti yetu Melvin Ayona, 7, aliyesomea Sasha Academy katika darasa la kwanza lakini namuachia Mwenyezi Mungu kwani ana mipango yake,” Bw Njairo akadokeza.

Aliongeza kwamba mali yake aliyofanikiwa kuokoa akishirikiana na mkewe iliporwa yote na kubakia na nguo alizokuwa amevalia!

Kakake marehemu Bw Atamo, aliyejitambulisha kwa jina Bw Samson Atambo, 50 alisema alikuwa na wakati mzuri na kakake jioni kabala ya mkasa.

“Alikuwa amenitembelea kwangu jioni kabla ya mkasa. Kwa hakika tulikuwa na wakati mzuri tukizungumza nisijue yatakayojiri baadaye. Aliniambia ana mipango ya kurudi mashambani kuishi kule kufuatia ukosefu wa kazi baada ya janga la Corona kuvuruga uchumi,” Bw Samson akanena.

Vilevile, Bw Samson aliongeza kwamba marehemu amewacha wanawe watatu mmoja wa kidato cha pili, mwingine darasa saba na wa mwisho kwenye darasa la pili.

Marehemu ni mzaliwa wa kijiji cha Tambe, tarafa ya Kiogutwa, divisheni ya Manga ilioko katika kaunti ya Nyamira.

Mkewe Bw Samson, Bi Pamella Kwamboka, 46 alisema alijulishwa kifo cha marehemu mwendo wa saa kumi na moja asubuhi ya jana.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Moses Mavesi ameomba serikali kujenga barabara za kutumika wakati wa dharura.

Moto huo ulizimwa na magari ya kuzima moto kutoka serikali ya kaunti lakini kwa shida kubwa kutokana na ukosefu wa njia.

Waathiriwa pia wanaomba misaada yoyote kutoka kwa wahisani kabla ya kuanza maisha upya.

Tukienda mitamboni Bw Mavesi alisema serikali imesimamisha ujenzi wa nyumba upya kutokana na sababu za usalama kwenye eneo la mkasa.

You can share this post!

Aibu wizara muhimu zikiburuta mkia katika ripoti ya...

Ramaphosa aomba utulivu wafuasi wa Zuma wakizua fujo