Wazazi kukamatwa kwa kuficha watoto wahalifu

Wazazi kukamatwa kwa kuficha watoto wahalifu

WAZAZI watakaoficha watoto wao ambao ni washukiwa wa uhalifu, watakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuwa washirika wa uhalifu.

Wakuu wa Usalama kaunti ya Mombasa wametaka wazazi kuwasalimisha watoto wao ambao wanashukiwa kuwa katika magenge yanayoendelea kuhangaisha wakazi na kutatiza amani.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw John Otieno, alisema mzazi atakayekosa kumsalimisha mtoto wake mhalifu ili arekebishwe tabia, atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuwa mshirika wa uhalifu.

“Kuna kisa kimoja ambapo maafisa wangu wa usalama walikuwa wanafuatilia walipofika kwenye sehemu ya uhalifu walimpata mzazi akimficha mwanawe mshukiwa wa uhalifu. Tulishangaa kugundua mtoto alikuwa amefichwa kwenye nguo,” alisema Bw Otieno, katika mkutano wa usalama Likoni.

Imebainika kuwa, baadhi ya watoto wanaojihusisha na uhalifu mitaani ni wenye umri mdogo kuanzia miaka 12.

“Maafisa wetu wa usalama wamejizatiti kulinda usalama, tunawaomba wakazi washirikiane nasi kukomesha utovu wa usalama,” alisema.

Wakati huo huo Bw Otieno aliwaamrisha machifu na manaibu wao kuchukua rekodi ya watoto wote wenye chini ya umri wa miaka 18 ambao hawaendi shuleni ili wazazi wao waeleze kinaga ubaga sababu za kutowapeleka shuleni.

“Kwa nini watoto wanarandaranda na shule ni bure? Watoto wote wanafaa kuwa shuleni. Wakienda shuleni hakuna yule atakayeshika silaha butu kukatakata watu na kutishia usalama,” alisema Bw Otieno.

Wakati uo huo, kamanda wa polisi Kaunti ya Mombasa, Bw Stephen Matu, aliwapa changamoto wakazi kutoa habari kwa vyombo vya usalama kuhusu uhalifu ili maafisa wa polisi waweze kuwakabili.

Katika kipindi cha miezi minne hivi wakazi wa Mombasa hasa maeneo ya Likoni, Kisuani na Nyali wameshuhudia utovu wa usalama huku magenge ya ujambazi yakichipuka upya.

Vyombo vya usalama pia vilitoa tahadhari kwa baadhi ya wanasiasa wanaosajili vijana kujiunga na makundi ya uhalifu.

You can share this post!

PAUKWA: Madhila ang’amua subira huvuta heri

ODM motoni kuacha Maitha katika mataa

T L