HabariHabari Mseto

Wazazi: Vitabu hivi vinawapotosha wanafunzi, viondolewe

March 7th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

WAZAZI Jumanne waliungana na walimu wa shule za sekondari kushinikiza kuondolewa kwa vitabu vipya vya Kidato cha Kwanza wanavyosema vinapotosha wanafunzi kutokana na makosa mengi.

Lakini kwa upande wao wachapishaji walijitetea vikali wakisema ni jukumu la walimu kurekebisha makosa wanayopata kwenye vitabu hivyo.
Hii inafuatia ufichuzi wa Taifa Leo hapo jana kuhusu vitabu vipya vilivyosambazwa na Serikali kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kuwa na makosa mengi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wazazi (KNAP), Bw Nicholas Maiyo alisema dosari zilizogunduliwa na walimu hazifai kupuuzwa zisije zikapotosha wanafunzi.

“Makosa yaliyomo ni makubwa na tunachukulia jambo hili kwa uzito. Inafaa vitabu hivyo viondolewe na utathmini wa kina ufanywe kwanza,” akasema Bw Maiyo aliongeza kuwa dosari zilizomo zinafanya mpango mzima wa vitabu bila malipo kukosa maana licha ya kugharimu Serikali Sh7.5 bilioni.

Mpango huo uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Januari 5, ulipelekea usambazaji wa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Kemia, Fizikia na Biolojia kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza waliojiunga na shule za upili za umma.

“Inatia wasiwasi sana kama wanafunzi watakuwa wanasoma mambo yenye makosa. Sasa tumeachia wizara iamue kile watakachofanya lakini pendekezo letu ni kuwa vitabu hivyo viondolewe darasani,” akasema.

Alishauri pia walimu wawe wakiripoti mapema wanapotambua kuna makosa kwenye vitabu ili vingine visichapishwe, na hali hiyo itatuliwe mapema.

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi. Picha/Jared Nyataya

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), Bw Akelo Misori alisema walimu walikuwa wameishauri Serikali ikague kwa kina vitabu hivyo kabla ya kuchapishwa lakini inaonekana ushauri wao ulipuuzwa.

Kulingana naye, asasi husika za serikali ziliharakisha shughuli hiyo iliyolenga zaidi kusaidia watoto wanaotoka katika familia maskini.

 

Jukumu la walimu

Kwa upande wake, Chama cha Wachapishaji Kenya (KPA) kilisema ni jukumu la walimu kufanya marekebisho wakiwa darasani hadi wakati matoleo mapya ya vitabu hivyo yatakapochapishwa baadaye.

Mwenyekiti wa KPA, Bw Lawrence Njagi aliondolea wachapishaji lawama akisema ni kawaida vitabu kuwa na makosa akisema makosa yaliyotajwa ni machache na hayataathiri elimu.

“Hakuna athari kwa mwanafunzi. Hii ndio sababu tuna walimu madarasani. Elimu inahusisha walimu, darasa, wanafunzi na vitabu. Mmoja wao akiondoka, hakuna elimu hapo. Ni jukumu la mwalimu kuelimisha na kufundisha vile inafaa,” akasema.

Kauli yake ilikosolewa na Bw Misori: “Inafaa ikumbukwe kuwa wanafunzi pia hujisomea wenyewe bila walimu kuwepo.

Kama watasoma mambo yenye dosari katika vitabu hivyo bila shaka watachanganyikiwa, na matokeo yao katika elimu yataathirika,” akasema na kuongeza kuwa walimu hawafai kulaumiwa kwa kosa lililotendwa na watu wengine na ambalo lingeepukika.

Mnamo Jumatatu, Mkuu wa Utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, alithibitisha dosari zipo na kusema utathmini unafanyiwa vitabu hivyo na hatua itakayochukuliwa itaamuliwa baadaye.