Wazazi wa ‘Metro Guy’ hawakutaka aende Uarabuni

Wazazi wa ‘Metro Guy’ hawakutaka aende Uarabuni

NA WINNIE ATIENO

KWA kipindi cha miaka mitatu, Abubakar Abbass, maarufu kama ‘Metro Guy’ alijaribu kusafiri Uarabuni kusaka kibarua ili kusaidia wazazi wake kutoka kwenye uchochole.

Hata hivyo, juhudi zake zilikuwa zinagonga mwamba kwa kuwa wazazi wake, Bi Warda Abbass na Bw Abbass Mwandambo, ambaye ni dereva wa malori ya masafa marefu, walimkataza wakihofia hatakuwa salama katika nchi hizo.

Licha ya kumsaidia kupata pasipoti, wazazi wake walikataa asisafiri hadi Uarabuni mara tano.

Sasa, baada yao kulegeza moyo na kumkubalia mwana wao kuenda kufanya kibarua Qatar, Abbass ameibuka kuwa fahari kubwa kwa wazazi wake wanaoishi mtaa wa Wayani, eneobunge la Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Kijana huyo alionekana kwenye video katika mitandao akielekeza mashabiki wa Kombe la Dunia mahali pa kuabiri basi maarufu kama ‘Metro’ nchini Qatar.

Hii ni baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 kuzoa sifa tele nchini Qatar wakati wa Kombe la Dunia linaloendelea.

Abubakar amesifiwa kimataifa kwa kufanya kibarua chake kwa njia ambayo iliwavutia na kuwafurahisha mashabiki wa Kombe la Dunia.

Katika video zilizoenezwa mitandaoni, Abubakar alionekana akizingirwa na mashabiki waliomshangilia kila alipotangaza ‘Metro, Metro’.

Mwandambo Abbass na mkewe Warda Abbass, wazazi wa nguli wa Kombe la Dunia la Qatar 2022 kijana Abubakr Abbass almaarufu Metro Man, wakati wa mahojiano eneo la Magongo, Mombasa, jana. PICHA|WACHIRA MWANGI

Umaarufu huo aliozoa ulimfanya kuangaziwa na mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa huku akialikwa kuhutubia mashabiki katika mojawapo ya mechi za Kombe la Dunia, ambapo alipata fursa ya kukaa pamoja na wageni wa heshima uwanjani.

“Kile wengi hawajui ni kuwa mtoto wangu amekuwa kijana mzuri sana, mcha Mungu na mwenye bidii. Alipopata umaarufu alinitumia video hizo akinieleza namna amejulikana kutokana na kazi yake. Hii yote ni sababu ya kumcha Mungu na bidii. Mungu anaweza kukuinua miongoni mwa watu milioni akakufanya maarufu,” alisema Bi Abbass huku akitoa dua.

Katika mtaa wa mabanda anakotoka Wayani, wazazi wake sasa wamebandiwka jina ‘Metro Metro’, ambayo ni matamshi yaliyomletea sifa kijana huyo.

Kwa mujibu wa wazazi wake, kijana huyo alikuwa akiamka asubuhi kumsaidia mamake kufanya kazi za nyumbani zikiwemo kuosha vyombo, kufagia na kupika kabla ya kwenda mazoezi ya kandanda.

Abubakar, ambaye ni mchezaji wa mpira shupavu katika timu ya Soweto FC mtaani kwao, huwa anafahamika kwa jina la kitani Aguero kutokana na umahiri wake katika kandanda unaowafanya wenzake kumfananisha na mwanasoka mashuhuri Sergio Aguero, wa Argentina.

“Nimekuwa maarufu sana kwa sababu ya mwanangu. Lakini hata zamani Abubakar alikuwa anajulikana sana kwa sababu ya kufungia mabao timu yake ya Soweto ambayo ilianzishwa na babake mkubwa mwaka wa 1970,” alifafanua babake.

Abubakar alisomea Shule ya Msingi ya Gome kabla ya kujiunga na ile ya upili ya Changamwe, alipopita na alama ya C katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Alikuwa ametamani kusomea kozi ya uhandisi katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa, lakini wazazi wake hawakuweza kugharimia karo na mahitaji mengine ya chuoni kwa sababu ya umaskini.

Badala yake, walimpeleka asomee udereva huku akiendeleza fani yake ya kandanda katika timu ya Soweto FC.

“Nilimwambia Mungu, heshima na hekima humpa hata yule mnyonge wa wanyonge ale meza moja na wafalme. Mwangalie jamani mtoto wangu. Alipopata umaarufu sikula wala kunywa maji siku nzima kwa sababu ya furaha,” akasema Bi Abbass kwenye mahojiano nje ya chumba cha Abubakar.

Abubakar ni kati ya Wakenya 3,600 kutoka eneo la Pwani waliotafutiwa nafasi za kazi Qatar kupitia kwa kampuni iliyoanzishwa na Mbunge Mwakilishi wa Mombasa, Bi Zamzam Mohamed.

Wazazi wake walitiwa moyo na diwani wa wadi ya Port Reitz ambaye pia ni naibu spika wa bunge la kaunti ya Mombasa, Bw Fadhili Makarani, kumruhusu mwanao akafanye kazi nje ya nchi.

“Alikuwa ameenda msikitini akasikia Bw Makarani akirai vijana kujisajili kufanya kibarua. Tulimruhusu baada ya kudadisi kila kitu, pia tulikuwa hatuna woga sababu Qatar ni tofauti na Saudi Arabia ambako watoto wetu wanateswa,” alisema babake.

Nahodha wa Soweto FC, Bw Mkala Anzafila, ambaye ni rafiki wa utotoni wa Abubakar alisema wanafurahi ameinua Mombasa ulimwenguni.

  • Tags

You can share this post!

Kundi C: Argentina na Poland kukabiliana kesho Jumatano

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Bruno Fernandes abeba Ureno dhidi...

T L