Habari za Kitaifa

Wazazi wajiandaa kuwapeleka watoto shuleni

January 4th, 2024 2 min read

NA FARHIYA HUSSEIN

UGUMU wa maisha unaendelea kuwabamiza Wakenya ukutani.

Baada ya kutamatika rasmi kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya 2024, sasa wazazi wanafanya matayarisho kuhakikisha watoto wanarejea shuleni.

Lakini wazazi wengi waliozungumza na Taifa Leo, wamesema ni kipindi cha kilio kwa sababu gharama ya maisha imepanda sana na hivyo bidhaa zinazohitajika shuleni kama vile sare na vitabu, bei imepanda ajabu.

Wazazi wameachwa kujikuna vichwa.

Matayarisho ya shule yameshamiri kila kona mjini mombasa wazazi wakihangaika na jua kali kutafuta sare na vitabu vya wanao dakika za lala salama kwa wanafunzi kurudi shuleni juma lijalo.

Katika duka maarufu la kuuza sare za shule la Mombasa Uniform kinyume na awali, tulipata idadi ya wateja ikiwa ndogo mno.

“Wakati ule wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kulikuwa kunashuhudiwa foleni ndefu na mteja alilazimika kusubiri wengine wapungue. Lakini sasa hakuna msongamano na hali hii inasababishwa na uchumi kudorora,” akasema Bw Ali Shariff, ambaye ni mmojawapo wa wazazi.

Mmiliki wa Mombasa Uniform Bi Monica Mutua alisema bado wiki moja shule zifunguliwe lakini wateja ni wachache.

“Watu wanakuja mmoja mmoja kulingana na vile kuko… mzazi anajiuliza atakuja ama atafanya nini,” akasema Bi Mutua.

Aliongezea pia walio kuwa ndani wako njia panda baada ya fedha walizokuja nazo kukosa kutosha.

Bw Shariff alisema wengine wametoka mbali Kinango huko wamekuja pesa hazitoshi inabidi warudi.

Vitabu vipya pia vimeonekana kupoteza hadhi hukuu wazazi wakiamua kununua vitabu vile kupunguza mzigo.

“Sasa shule zinatuambia vitabu tununuwe wenyewe. Tunatakiwa tununue sare. Kiukweli hali ni tofauti ukilinganisha na nchi jirani ya Uganda,” akasema Bw Shariff.

Mzazi mwingine, Bi Roselyne Riga, alisema watu wengi wanaenda kununua kwa wauzaji wa vitabu chakavu.

Licha ya kuwa watu wengi wanafurika hapa kununua vitabu vilivyotumiwa, bei imepanda ambapo wauzaji wanalalamikia kupungua kwa wateja.

Kulingana na muuzaji wa vitabu Bi Ann Wairimu, “biashara iko chini kidogo… si kama hapo awali na bei imepanda kiasi ambapo kitabu tulichokuwa tukiuza kwa Sh500 sasa tunakiuza kwa Sh700.

Kwa wanafunzi wanaosomea katika shule za mbali, nauli inawatatiza kwani magari mengi ya uchukuzi wa umma yamepandisha nauli.

Wazazi na wauzaji sasa wameitaka serikali kuingilia kati hasa kuhusu swala la ununuzi wa bidhaa za shule na bila shaka kupunguza gharama ya maisha.