Wazazi walia kanuni za corona zinaumiza watahiniwa wa KCSE

Wazazi walia kanuni za corona zinaumiza watahiniwa wa KCSE

NA MWANGI MUIRURI

Muungano wa wazazi katika Mlima Kenya Jumatatu umeteta kuhusu hatua ya serikali ya kuzima usafiri kutoka Kaunti ya Murang’a hadi ya Kiambu na pia hadi Kaunti ya Machakos ukisema ni wazo ambalo halikutilia maanani wanafunzi ambao wanavuka mipaka hiyo hadi shuleni kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.

Katibu wa muungano huo Bi Cecilia Kamande alisema kuwa “licha ya kuwa tunafahamu kwamba rais alizima usafiri huo ndio apambane na makali ya ugonjwa wa Covid-19 unaoletwa na virusi vya Corona, angefafanua zaidi kuhusu wanafunzi hao.”

Bi Kamande alisema kuwa kuna wanafunzi wa kidato cha nne ambao husafiri shuleni kila asubuhi na kwa wakati huu KCSE inaendelea mbele kufanywa, ingekuwa busara kwa Rais Kutoa mwelekeo wa kina kuwahusu.

Makataa hayo ya usafiri yalianza kutekelezwa Jana usiku mwendo wa saa mbili, leo ikiwa ni siku ya pili ya mtihani huo ambao ulianza Ijumaa.

Kaunti ya Murang’a ni jirani kwa Kaunti za Machakos na Kiambu ambapo katika mipaka huwa na uvukaji wa hali za kibiashara, masomo, dini na pia ule tu ujirani wa kawaida.

Naibu Waziri wa Spoti Bw Zack Kinuthia (aliye na koti la Samawati) akiongea Jumapili na wadau wa elimu katika Kaunti ndogo ya Kandara. Picha/ Mwangi Muiruri

Rais alizima usafiri wa kuingia au kutoka Kaunti za Kajiado, Machakos, Nairobi, Kiambu na Nakuru kwa wakati ambao haukubainika, muungano huu wa wazazi ukisema kuwa hali ya kutatiza wanafunzi itajiangazia katika mipaka ya Kaunti hizo zilizo jirani na zilizotambuliwa kama zilizoathirika zaidi na Covid-19.

Bi Kamande alisema kuwa makataa hayo licha ya kutatiza wanafunzi katika hekaheka za kusaka uchukuzi hadi shuleni, pia imewatia taharuki ya ugonjwa, hali ambayo inaweza ikaathiri fikira zao na kuishia kuwafanya wafeli mtihani.

“Haya makataa ya uchukuzi yatawatwika wazazi mzigo mkubwa wa nauli kwa kuwa magari yatapandisha bei. Huenda pia kuwe na ufisadi katika vizuizi vya barabara ambapo wanafunzi hawa watahitajika kutoa hongo ndio wavuke. Hatimaye, ni tangazo ambalo limezua wasiwasi mkuu hapa nchini kwamba Kaunti ambazo aliorodhesha ni kama jangwa la mauti hivyo basi ni lazima litaathiri fikira za wanafunzi,” akasema.

Bi Kamande aliitaka serikali kuwapa wanafunzi wote pasi spesheli za kuwawezesha kuvuka mipaka bila kutatizwa na maafisa wa kiusalama na pia iwape ushauri nasaha kwamba sio eti kumeharibika kiasi kwamba hiyo mipaka ni ya kuingia kwa jangwa la mauti.

Bi Michele Muthoni ambaye ni mzazi amtaka Rais aamrishe Watahiniwa wa KCSE wanaovuka mipaka ya Kaunti zilizozimiwa utangamano juu ya Covid-19 hawatazuiliwa katika vizuizi vya polisi. Picha/Mwangi Muiruri

Aliwataka wahudumu wa matatu pia waelewe kuwa wanafunzi hao wanahitaji kuungwa mkono ili wamalize mtihani wao kwa amani “hivyo basi kuwaongeza nauli kiholela ni sawa na kukimbizana na faida za haramu kupitia kuwafanyia biashara watoto katika mazingara ya janga la kitaifa.”

You can share this post!

Jambazi sugu Maragua aponea kuuawa na polisi baada ya...

Naibu Waziri aishangaa sekta ya matatu kunyima vijana...