Habari MsetoSiasa

Wazazi walipie miradi ya shule, serikali haina pesa – Magoha

June 11th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

SERIKALI haina pesa za kusaidia shule za sekondari kukidhi mahitaji ya uhaba wa miundomsingi, Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema.

Kutokana na hali hiyo, Prof Magoha amewataka walimu kuwatwika wazazi mzigo wa kufadhili mahitaji kama vile ujenzi wa madarasa mapya, vyumba vya malazi, kuajiri walinzi, wapishi na kununua madawati.

Akizungumza katika kongamano la 44 la walimu wakuu wa shule za upili, Prof Magoha alisema tayari serikali imetenga asilimia 35 ya bajeti yake kusimamia sekta ya elimu, kwa hivyo hakuna uwezekano wa kuongezewa pesa zaidi.

“Kuna wizara nyingi ambazo zinagawana asilimia 65 baada elimu kutengewa asilimia 35. Mbona walimu wakuu wasiwaombe wazazi wanaojiweza kifedha kutoa michango, ili kuboresha shule kwa manufaa ya watoto wao?” akauliza Prof Magoha.

Kulingana na sheria za Wizara ya Elimu, shule hazipaswi kuitisha walimu fedha zozote isipokuwa za malazi na chakula.

Lakini licha ya kutaka wazazi wahusishwe katika kufadhili upanuzi wa miundomsingi, Prof Magoha aliwaonya walimu wakuu dhidi ya kuwafukuza watoto nyumbani wazazi wanapokosa kulipa fedha hizo.

“Sitaki kusikia mwanafunzi amefukuzwa shuleni kwa ajili ya miradi hii. Hiyo ni michango ya hiari ambayo haipaswi kulazimishiwa wazazi,” Prof Magoha akasema.

Pia aliwashauri walimu wakuu wawe wakinunua bidhaa za shule moja kwa moja sokoni wala si kutegemea wafanyibiashara.

“Kama mwalimu mkuu, nenda sokoni ukahakikishe bei za bidhaa. Baadhi ya watu mnaowatuma ni wezi ambao wanawaibia pesa kwa kupandisha bei za bidhaa,” akasema.

Kuhusu masuala ya kuongeza idadi ya walimu shuleni, waziri alisema tayari serikali imetenga fedha za kutosha ili kupunguza uhaba mkubwa wa walimu unaokumba shule za umma.

Prof Magoha pia aliwaonya wahusika wa bima ya afya nchini dhidi ya kuwanyima wanafunzi huduma kwa kisingizio cha kutokuwa katika mfumo wa usajili wa dijitali.

“Kila mwanafunzi ana haki ya kupata bima hii kwa sababu serikali imewahesabu wanafunzi wote nchini. Kwa hivyo kuwanyima huduma za matibabu kutakuwa ni kukiuka sheria, na mhusika atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.