Makala

Wazazi wanadhuru watoto kwa kunywa pombe nyumbani

August 18th, 2020 6 min read

Na LEONARD ONYANGO

[email protected]

KUFUNGWA kwa baa na maeneo ya burudani kumewaweka wazazi wanaopenda kubugia mvinyo kwenye kona mbaya.

Tofauti na hapo awali, ambapo siku za wikendi wazazi walikwepa watoto na kwenda kunywa pombe kwenye baa huku wakitazama mechi za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyo na ushabiki mkubwa humu nchini, sasa hawana pa kujificha.

Wazazi hao sasa wamelazimika kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa wanaendelea kukata  kiu cha pombe.

Bw George Otieno ambaye ni mkazi wa mtaa wa Dandora jijini Nairobi anasema kuwa amelazimika kugeuza gari lake kuwa ‘baa’.

Anasema siku za wikendi ambazo haendi kazini, huwa ndani ya gari lake akinywa pombe.

“Sitaki watoto wangu wajue kwamba mimi hutumia mvinyo. Mimi hunywa pombe ya kadri tu na watoto wangu huwa hawana habari kwamba baba yao ni anatumia pombe, hawajawahi niona  nikinywa,” anasema Bw Otieno ambaye ni baba ya watoto watatu.

“Ukiwaeleza kwamba baba yao ni mlevi watakushangaa sana,” anaongezea.

Naye Eric Mbugua ambaye ni mkazi wa Kahawa West, Nairobi, anasema kuwa pombe anayonunua amehifadhi kwenye chumba chake cha kulala.

“Nina watoto wawili; mmoja ana umri wa miaka 10 na mwingine miaka 13. Watoto wangu hawana mazoea ya kuingia kwenye chumba cha kulala cha wazazi wao. Nimewafunza hivyo tangu walipokuwa  wachanga. Hivyo pombe yangu chumbani iko salama.

“Siku za wikendi, mimi hujifungia chumbani kwangu na kunywa pombe huku watoto wakijisomea au kutazama runinga sebuleni na mama yao ambaye hatumii mvinyo,” anasema.

Vileo vinavyotumiwa na watoto:

Pombe- asilimia 23

Miraa- asilimia 17

Tumbako- asilimia 15

Bangi- asilimia 8

Heroini- asilimia 1

Kokeni – asilimia 1

Katika eneo la Huruma jijini Nairobi, Willy Makokha anasema kuwa yeye na mkewe wamekuwa wakibugia pombe tu mbele ya watoto wao wawili.

“Tunaishi kwenye chumba kimoja. Chumba hicho ndicho sebule na sehemu ya kulala. Unajua nyumba hizi za mjini, haswa vitongoji duni, hazina maeneo ya kupumzika nje. Makarao (maafisa wa polisi) wakikupata unakunywa pombe nje wanakushika.

“Kuepuka balaaa ya kukamatwa, nanunua pombe yangu dukani na ninakunywa hapa chumbani kwangu,”anasema Bw Makokha anafanya kazi ya useremala mtaani Huruma.

Kulingana na Makokha, watoto hawawezi kuiga wazazi wao kunywa pombe.

“Mimi wazazi wangu hawakuwa wanakunywa pombe, lakini mimi ninakunywa. Hivyo watoto wangu watafanya uamuzi wao wenyewe wakiwa wakubwa. Kwa sasa nawahimiza kutia bidii katika masomo yao ili wajisaidie katika siku za usoni,” anasema.

Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita alipiga marufuku kuuzwa kwa pombe katika baa, mikahawa na maeneo ya burudani. Rais Kenyatta pia alifunga baa kwa muda usiojulikana.

Rais Kenyatta alisema kuwa watu watumiaji wa pombe wanaweza kununua mvinyo madukani na kwenda kunywea nyumbani.

Wito huo wa Rais Kenyatta, unapingwa vikali na Mamlaka ya Kupambana na  Matumizi ya Dawa za Kulevya nchini (Nacada).

Watoto hutumia vileo wakati upi?

Likizo – asilimia 49

Njiani kutoka shuleni kwenda nyumbani – asilimia 36

Wikendi – asilimia 30

Ziara za wanafunzi = asilimia 27

 

Mamlaka ya Nacada linaonya kuwa hatua ya wazazi kunywea pombe nyumbani itasababisha watoto kujiingiza katika ulevi.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa  Nacada Mabel Imbuga  pia anasema kuwa tangu kufungwa kwa baa pombe imekuwa ikiuzwa kupitia mitandaoni hivyo  watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kuipata bila kizuizi.

“Baadhi ya wanafunzi wanatumia mitandao kusoma hivyo wanaweza kutumia fursa hiyo kununua pombe bila wazazi wao kujua,”anasema.

“Kunywa pombe nyumbani kuna wanyima watoto mazingira bora na salama ya kusomea na kuishi wakati huu wa janga la virusi vya corona. Tunawashauri wazazi kutumia wakati huu kujiepusha na pombe na badala yake wajenge uhusiano wa karibu na watoto wao. Wazazi ndio wametwikwa jukumu la kuwalinda watoto wao hivyo ni sharti wawalinde dhidi ya mazingira yenye pombe,”anasema Prof Imbuga.

Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia wanaonya  kuwa kunywa pombe nyumbani mbele ya watoto kuna madhara tele.

Bi Dorcas Okinyi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya afya ya akili na mwasisi wa shirika la Healthy Minds Africa, anasema kuwa watoto huanza kutambua harufu ya pombe wakiwa na umri wa kati ya miaka mitatu na mitano.

“Watoto huanza maisha yao kwa kutangamana na watu katika familia zao. Watoto hujifunza na kuiga tabia fulani kwa kuangalia au kusoma watu wanaotangamana nao na  huchukulia wazazi wao kama kielelezo.

“Idadi kubwa ya watoto wanaoona wazazi wao wakinywa pombe wao pia huishia kuwa walevi baadaye na kupitisha tabia hiyo kwa kizazi kingine,” anasema.

Watoto hupata  wapi  vileo?

Marafiki – asilimia 32

Nyumbani- asilimia 29

Vibanda vilivyo karibu na shule – asilimia 25

Jamaa zao- asilimia 17

Wazazi – asilimia 8

 Bi Okinyi anasema kuwa hali huwa mbaya zaidi kwa watoto wazazi au walezi wao wanapolewa chakari na kuzua vurugu nyumbani.

“Wazazi wanapokunywa pombe na kuzua vurugu, watoto huathirika sana kiakili. Hiyo ndiyo maana watoto wa wazazi walevi huwa na matatizo ya kutangamana na wenzao shuleni au wanapocheza mitaani; wengi wao huepndelea kupigana.

“Mzazi anapolewa ndani ya nyumba na kuzua vurugu au kusumbua majirani, pia husababisha kuwa na tabia ya kuepuka wenzao kutokana na aibu. Hali hii humfanya mtoto kuwa na matatizo ya kiakili,” anasema.

Vilevile, Bi Okinyi anasema kuwa watoto wanaaishi kwa hofu iwapo mzazi au mlezi huwadhuru kwa kuwapiga baada ya kulewa.

“Watoto hujawa na hofu wanapokuwa nyumbani kwani hawajui watafanyiwa nini na mzazi au mlezi wao baada ya kulewa,” anasema.

“Hali hiyo huwafanya kuchukia mzazi au mlezi wao ambaye ni mlevi na hatimaye kukumbwa na msongo wa mawazo ambao unaweza kuwasukuma wao pia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya,”anaongezea.

Je, nini hutokea ikiwa wazazi wanakunywa pombe  nyumbani kwa ustaarabu bila kuzua vurugu au kudhuru watoto wao?

Bi Okinyi anasema kuwa hata kunywa pombe kwa ustaarabu mbele ya watoto hakufai.

“Kuna baadhi ya wazazi ambao wanakunywa pombe kiungwana lakini wanaonya watoto wao wasithubutu kuweka mvinyo mdomoni.

“Hili husababisha watoto kuwa na shauku ya kutaka kuonja pombe ili washuhudie ‘utamu’ ambao wazazi wao hupata kwenye pombe. Kuonja huku husababisha watoto kuwa walevi chakari katika siku za usoni,” anasema Bi Okinyi.

“Wazazi hawafai kuwataka watoto wao kunywa maji na wao wanakunywa pombe. Wazazi wanafaa kuwa kielelezo bora kwa watoto wao,”anaongezea.

Watoto wanaotumia mihadarati wanaishi na nani?

Mama na baba- asilimia 70

Mama pekee – asilimia 17

Baba pekee – asilimia 3

Nyanya/babu- asilimia 2

 

Anasema kuwa watoto huiga zaidi mambo wanayoona kwa wazazi au walezi wao kuliko wanayosikia.

Bi Okinyi anashauri kuwa wazazi wanaokunywa pombe nyumbani wanafaa kuwaelimisha watoto wao kuhusu madhara ya kubugia mvinyo.

“Mzazi anaweza kumshauri mtoto kuhusu madhara ya kunywa pombe huku akitoa mfano wake kuhusu mambo yaliyomsukuma kufanya hivyo na changamoto anazopitia,” anasema.

“Mzazi anayetumia pombe anafaa kuzungumza na watoto kwa uwazi kuhusu madhara ya pombe badala ya kuwapa onyo kali na  kuwatishia kuwaadhibu iwapo watathubutu kunywa vileo. Watoto wanahitaji kuelezwa ni kwanini wanafaa kujiepusha na pombe  kabla ya kukamilisha masomo yao ya shule ya msingi na sekondari.”

Anawashauri wazazi walio na mazoea ya kulewa chakari mbele ya watoto kutafuta huduma za ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.

Prof Imbuga anasema kuwa wazazi walio na matatizo ya kulewa chakari wanaweza kuwasiliana na Nacada ili wapewe ushauri kuhusu namna ya kupata matibabu.

 Wataalamu wanaamini kuwa unywaji wa pombe nyumbani umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la visa vya dhuluma dhidi ya watoto wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Adhabu ya kumweka mtoto kwenye mazingira yanayomweka kwenye hatari ya kutumia vileo

Miezi 12 gerezani

Faini ya Sh50,000

Rais  Uhuru Kenyatta mwezi  uliopita aliagiza kufanywa kwa uchunguzi ili kunasa watu anaohusika na dhuluma dhidi ya watoto na wanawake.

Agizo hilo lilifuatia baada ya  wizara ya masuala ya Jinsia kufichua kuwa visa vya ubakaji wa wanawake, unajisi wa wasichana na mizozo ya nyumbani imeongezeka mara 10 kati ya Aprili na Julai ikilinganishwa na Februari mwaka huu.

Ripoti zinaonyesha kuwa  visa vingi vya ubakaji na unajisi vinatekelezwa na jamaa za waathiriwa.

Utafiti uliofanywa na Nacada  miongoni mwa shule za msingi mnamo 2016, ulifichua kuwa wazazi wanachangia pakubwa katika kuwaingiza watoto wao katika utumiaji wa vileo.

Utafiti huo ulifichua kuwa pombe ndiyo hutumiwa kwa wingi miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka 17 ikilinganishwa na aina nyinginezo za vileo.

Kwa mujibu wa ripoti, pombe hutumiwa kwa asilimia 23, miraa (17), tumbako (15), bangi  (8), heroini (1), kokeni (1) kati ya aina nyinginezo za vileo..

Asilimia 48.5 ya watoto hutumia mihadarati wakati wa likizo na wengine asilimia 35.1 wanatumia njiani wanapotoka shuleni kuelekea nyumbani. Ripoti pia ilibaini kuwa asilimia 30 ya watoto hutumia vileo siku za wikendi, asilimia 27 hunywa pombe na vileo vingine wakati wa ziara za wanafunzi.

“Wanafunzi hao walipoulizwa mahali ambapo hutoa vileo hivyo, asilimia 32 walisema kuwa huwa wanapewa na rafiki zao. Jambo la kushangaza ni kwamba asilimia 29 walisema kuwa hutoa nyumbani,” ikasema ripoti hiyo.

Asilimia 25 walisema kuwa hununua vileo hivyo katika vibanda vilivyo karibu na shule, asilimia 17 walisema hupewa na jamaa zao na asilimia 8 walikiri kuwa walipata kutoka kwa wazazi wao.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, asilimia tano ya wanafunzi waliohojiwa na Nacada walisema kuwa hupata mihadarati hiyo kutoka kwa walimu huku wengine asilimia nne wakisema hununua katika maduka yaliyo ndani ya shule.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba karibu asilimia 70 ya wanafunzi waliokiri kutumia mihadarati wanaishi na wazazi wao wote wawili. Asilimia 17 wanaishi na mama tu huku wengine  asilimia 3 wakiishi na baba pekee.

Katika mapendekezo yake, Nacada iliwataka wazazi kuepuka kunywa pombe mbele ya watoto wao.

“Wazazi pia wanafaa kusindikiza watoto wao hadi shuleni ili kuwazuia kushawishiwa na wenzao kutumia mihadarati wanapokuwa njiani kuelekea shuleni,” inapendekeza ripoti ya Nacada.

Ripoti pia inashauri wazazi kuwa na midahalo na watoto wao  kuhusu suala la mihadarati.

Sheria ya Watoto ya 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2012, inasema kuwa kila mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya dawa za kulevya kama vile tumbaku, mihadarati, pombe. Sheria hiyo pia inapiga marufuku watoto kutumiwa kuzalisha au kusafirisha vileo.

Wazazi au mtu yeyote anayepatikana na hatia ya kuwaweka watoto katika mazingira ya vileo anakuwa katika hatari ya kufungwa kipindi kisichozidi miezi 12 gerezani au kutozwa faini isiyozidi Sh50,000.