Habari Mseto

Wazazi watakiwa kuripoti visa vya watoto kunajisiwa na watu wa familia

April 9th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

IDADI ya visa vya watoto wadogo wanaonajisiwa kwa kubakwa na kulawitiwa katika kaunti ya Lamu inaibua maswali mengi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kutetea Haki za Waislamu (MUHURI) tawi la Lamu, zaidi ya watoto 10 hudhulumiwa kingono kila mwezi bila ya waathiriwa kupata haki.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Jumatatu, maafisa wa MUHURI walisema cha kusikitisha zaidi ni kwamba watoto wengi wanaopitia madhila hayo huishia kufichwa na wazazi badala ya visa hivyo kuangaziwa ili waadhiriwa wapate haki.

Afisa Mkuu wa MUHURI eneo hilo, Bi Ummulkher Salim, alisema aghalabu wanaotekeleza vitendo hivyo kwa watoto husika ni wale wa uhusiano wa karibu, ikiwemo wajomba, mabinamu na pia akina baba wa watoto hao.

Alitaja sehemu za Tchundwa, Kiunga, na mji wa kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo ambapo visa vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo vinaendelezwa kisiri.

Mwenyekiti wa CIPK tawi la Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe. Amelaani vikali ubakaji na ulawiti wa watoto eneo la Lamu, akisema vitendo hivyo ni kinyume cha dini. Ataka wahalifu kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Picha/ Kalume Kazungu

Kwa mujibu wa Bi Salim, wazazi wamekuwa wakichangia pakubwa kukithiri kwa vitendo hivyo kutokana na kwamba wengi wao hukimbilia kutatua uhalifu huo kijamii badala ya kuwaripoti wahalifu ili wakabiliwe na mkono wa sheria.

“Ni masikitiko makuu kwamba watoto wengi hapa Lamu wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa. Cha ajabu ni kwamba watu wa ukoo ndio mara nyingi hutekeleza vitendo hivyo. Hii ndiyo sababu wazazi wanakimbilia kutatua matatizo hayo kijamii badala ya kuhakikisha wahalifu wamekabiliwa na mkono wa sheria,” akasema Bi Salim.

Naye Naibu Afisa wa MUHURI eneo la Lamu, Bw Ali Habib, alisema shirika hilo tayari limeanzisha mpango wa kufadhili kesi kwa waathiriwa wa vitendo hivyo.

Kulingana na Bw Habib, wazazi wa waathiriwa au waathiriwa wenyewe wanahimizwa kuripoti visa hivyo kwa ofisi ya MUHURI ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka dhidi ya wanaotekeleza vitendo hivyo.

Naibu Afisa wa MUHURI tawi la Lamu, Ali Habib wakati wa mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake. Picha/ Kalume Kazungu

Wazazi wapige ripoti 

“Lengo letu kama MUHURI ni kuhakikisha haki imepatikana kwa watoto wanaofanyiwa unyama huo. Tunawahimiza  wazazi wa watoto husika kupiga ripoti kwa ofisi yetu.

Kama shirika, tutachukua malalamishi yao kisiri bila ya kumtaja yeyote atakayeripoti kwetu. Tuko tayari kudhamini kesi kama hizo na kuona kwamba haki imepatikana na visa hivyo vinakomeshwa kabisa eneo la Lamu,” akasema Bw Habib.

Wakati huo huo, Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) tawi la Lamu limelaani vikali vitendo hivyo dhidi ya watoto eneo hilo.

Mwenyekiti wa CIPK tawi la Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe aidha alipinga vikali madai kwamba kutoripotiwa kwa visa kama hivyo kunatokana na utamaduni wa kale pamoja na misingi ya dini ya kiislamu kwa wakazi wa Lamu.

Aliwashauri wazazi kutowaficha majumbani watoto wao punde wanapodhulumiwa.

“Kubakwa au kulawitiwa kwa watoto ni kinyume kabisa cha dini. Wanaotekeleza uhalifu huo sharti waandamwe kisheria. Dini inakataza zinaa na kufanywa kwa vitendo kama hivyo kwafaa adhabu kali,” akasema Ustadh Shekuwe.