Habari Mseto

Wazazi, watoto waelezwa njia za kufuata mkondo bora maishani

June 22nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa makanisa wamewahimiza vijana wajiepushe na maovu na badala yake kufuata mkondo bora wa kuwa tegemeo siku za usoni.

Naye Mbunge wa Thika amewahimiza wazazi wawe makini na wana wao ili wasije wakaangamizwa na dawa za kulevya.

Mchungaji wa Kanisa la Chrisco Church, Magogoni, Thika Bw Simon Mbatia, alisema kanisa ni eneo takatifu laMwenyezi Mungu, wala sio mahala pa kuzungumzia maswala ya siasa holela.

“Sisi kama wachungaji tunataka kuweka wazi kuwa tunataka kusambaza neno la Mungu kanisani lakini sio kukubalia viongozi kurushiana cheche za matusi,” alisema Bw Mbatia.

Alisema cha muhimu kwa wakati huu ni viongozi kuzingatia maendeleo hadi mwaka wa 2022 ili wananchi wapate maendeleo walioahidiwa nao.

Aliyasema hayo Ijumaa katika kongamano la wachungaji 120 wa madhehebu mbalimbali kutoka Kaunti ya Kiambu lililofanyika kituo cha mafunzo cha Kolping, Kilimambogo, Thika Mashariki.

Kamari

Lilihudhuriwa pia na Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliyetoa mwito kwa wazazi kuwalinda wana wao kujiepusha na uchezaji wa kamari na dawa za kulevya.

Alisema familia nyingi zimepoteza matumaini kwa sababu ya msongo wa mawazo.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, akagua nguo zinazoshonwa na wanafunzi wa chuo cha Kolping’, Kilimambogo, Thika Mashariki. Aliandamana na Mchungaji wa Kanisa la Chrisco Church, Bw Simon Mbatia. Picha/ Lawrence Ongaro

“Siku hizi vijana wengi wamepoteza mwelekeo kwa kujiingiza kwa uchezaji wa kamari na kusahau kufanya kazi kwa bidii. Wengi wanaamini kutajirika kwa haraka,” alisema Bw Wainaina.

Aliwaomba wachungaji kuwa mstari wa mbele kuzipatia ushauri familia nyingi zilizo na shida za kifamilia.

“Siku hizi tunashuhudia kesi nyingi za watu kujinyonga kwa sababu ya matatizo ya kifamilia. Kwa hivyo, ni vyema wachungaji kujitokeza kuwapa ushauri wa kiroho,” alisema Wainaina.

Alisema huu ni wakati wa kuchapa kazi wala sio wakati wa kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Iwapo tutafanyia wananchi kazi ipasavyo bila shaka watapata nafasi nzuri ya kuchagua viongozi wao ifikapo wakati huo,” alisema Bw Wainaina.

Askofu wa Kanisa la Regeneration Evangelistic Church Bw Francis Maina aliwahimiza viongozi wafuate maagizo ya Rais Uhuru Kenyatta ya kufanyia wananchi kazi.

“Iwapo mwongozo huo utafuatwa bila shaka mwananchi wa kawaida atakuwa amefaidika pakubwa na maendeleo,” alisema Askofu Maina.