Makala

Wazee: Kudorora kwa uchumi Mlima Kenya ndio chanzo cha Mungiki ‘kufufuka’

January 3rd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KUCHIPUKA upya kwa kundi la Mungiki katika eneo la Mlima Kenya kumezua maswali kuhusu sababu ambazo huenda zimechangia kurejea kwa kundi hilo hatari.

Kundi hilo lilichipuka mapema 2000, msingi wake ukiwa “kutetea na kurejesha utamaduni wa jamii ya Agikuyu” ambao waanzilishi wake walisema “ulikuwa ukitishiwa na wimbi la tamaduni za Kimagharibi”.

Waanzilishi wake wakuu walikuwa ni Bw Maina Njenga, Bw Ndura Waruinge (ambaye ni binamuye Bw Maina), marehemu Ngonye wa Gakonye kati ya wengine wengi.

Ijapokuwa serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki ilifanikiwa kulikabili vikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, marehemu John Michuki mnamo 2007, kundi hilo sasa limeanza kufufuka upya katika eneo hilo.

Wanachama wake wameripotiwa kufanya matambiko katika maeneo kadhaa ya Mlima Kenya, hasa kaunti za Nyeri na Murang’a.

Ni hali ambayo imemfanya Naibu Rais Rigathi Gachagua kujitokeza wazi na kutangaza kwamba amewaagiza maafisa wa usalama katika eneo la Kati na Mlima Kenya kwa jumla, kuhakikisha kuwa hakuna mkutano wowote wa kundi hilo unaoruhusiwa kufanyika.

“Hatuwezi kuruhusu urejeo wa kundi hilo katika eneo hili. Tutakumbuka kwa machungu ukatili lililowafanyia watu wetu katika maeneo tofauti nchini. Nimewaagiza maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa hakuna shughuli zozote zinazohusiana na kundi hilo zinazoruhusiwa kufanyika katika eneo hili,” akasema Bw Gachagua.

Licha ya onyo hilo kali, wadadisi, wazee na viongozi tofauti kutoka ukanda huo, wanataja kudorora kwa hali ya uchumi nchini kama chanzo kuu cha kurejea kwa kundi hilo.

“Wakati kundi hilo lilipoanzishwa mara ya kwanza, misukumo yake ilikuwa sababu za kiuchumi na kitamaduni. Waanzilishi wake walilenga kuishinikiza serikali kuanzisha mipango ya kuwapa ajira vijana kutoka Mlima Kenya. Pili, lililenga kutetea udumishaji wa tamaduni na desturi za jamii ya Agikuyu,” asema mdadisi wa siasa Maina Gikandi.

Anasema kuwa sababu zilizoonekana kuchangia kuanzishwa kwa kundi hilo ndizo zinaonekana kuwasukuma viongozi kama Maina Njenga kulifufua upya.

“Gharama ya maisha imepanda na vijana wengi hawana ajira kwa sasa. Wanalazimika kuwatoza ada wafanyabiashara katika eneo hilo ili kujikimu kimaisha. Bila shaka, hilo linaashira ukosefu wa ajira miongoni mwao,” akasema.

Kulingana na mwanasiasa mkongwe Koigi wa Wamwere, ambaye kwa wakati mmoja alihudumu kama mbunge wa Subukia, Kaunti ya Nakuru, mchipuko mpya wa kundi hilo unafaa kuizindua serikali kushughulikia ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

“Maasi dhidi ya serikali na utawala uliopo huanza kwa mchipuko wa makundi kama hayo. Hii ni nafasi kwa serikali kutatua changamoto zilizopo, japo pia hilo halifai kuwafanya vijana kuanza kujiingiza kwenye uhalifu,” akasema Bw Wamwere.