Habari Mseto

Wazee kukagua 'muratina' ya kutumika katika sherehe

January 18th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI itazidi kupambana na pombe haramu katika kaunti ndogo ya Gatundu Kaskazini.

Naibu kamishna wa eneo hilo Bw Buxton Mayabi alisema atashirikiana na wazee wa vijijini na machifu ili kukabiliana na janga hilo.

Hata hivyo pombe ya kienyeji ya wazee ya muratina itaruhusiwa kupikwa tu wakati wa sherehe za jamii ya Agikuyu.

“Tumekubaliana na wazee ya kwamba kwa sababu ya mila za Agikuyu tutakubalia wazee walioteuliwa na wazee wa Kiama kupika pombe hiyo itakayokaguliwa na chifu na wazee hao kama inakubalika,” alisema Bw Mayabi.

Alisema wale watakaopika pombe hiyo bila kupata kibali kutoka kwa wazee wa kiama watatiwa nguvuni na kushtakiwa.

“Hatutaki ionekane kama pombe hiyo imehalilshwa lakini hiyo itapikwa kukiwa na karamu inayotambulika kijijini na jamii nzima,” alisema Bw Mayabi.

Alisema siku chache zilizopita mkazi mmoja wa eneo hilo alinaswa na lita 400 za pombe ya ‘muratina’ huku akisema ni ya sherehe.

Baadaye mshukiwa huyo alipelekwa mahakamani na kukanusha mashtaka ambapo alipewa dhamana ya Sh 100,000, huku akijiandaa kuendelea na kesi hiyo.

Aliyasema hayo Alhamisi, eneo la Kamwangi, Gatundu Kaskazini, alipofanya mkutano kwenye afisi yake na wazee wa kiama kutoka vijiji 28 vinavyotambulika kirasmi.

Wazee wengi waliohudhuria mkutano huo walikubaliana kwa kauli moja ya kwamba hakuna mkazi yeyote atakayekubaliwa kupika pombe haramu katika eneo hilo.

 

Wazee wa Kiama eneo la Kamwangi wasikiliza mzungumzaji mmoja Januari 14, 2020. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati wa mkutano huo, wazee zaidi ya 30 waliteuliwa ili kusimamia upikaji wa pombe hiyo katika sherehe na kuhakikisha hakuna kemikali mbaya inawekwa ndani.

Mlezi na Mwenyekiti wa kikundi hicho cha wazee Bw Joseph Mbiruri Waweru, alisema kwa muda mrefu wameshirikiana vyema na naibu Kamishna Bw Mayabi na wataendelea kufanya hivyo ili kukabiliana na watu wanaopika pombe haramu.

“Sisi kama wazee wa Kiama hatutakubali watu wachahe watuharibie sifa kwa kupika pombe mbaya ya ‘muratina’ inayoweza kumdhuru mtu. Lengo kuu ni kutengeneza pombe kidogo ya wazee ambayo imetambulika tu na wazee wakati wa sherehe za Agikuyu,” alisema Bw Waweru.

Mzee mwingine wa kiama Bw Gichuhi Ndung’u, alisema wao kama wazee wanaoheshimika katika eneo la Gatundu na vitongoji vyake hawatakubali walaghai waje kupika pombe haramu ili kujitajirisha.

“Tunajua kuna watu wengine watajifanya eti wanapika pombe ya muratina lakini nasi kama wazee tukiwapata tutawachukulia hatua kali kama wazee wa kiama,” alisema Bw Ndung’u.