Wazee kumbariki Ruto huku Gideon akibaki na rungu

Wazee kumbariki Ruto huku Gideon akibaki na rungu

Na ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto anaanza leo safari yake ya kuelekea Ikulu huku akizindua rasmi kampeni zake. Baada ya uzinduzi huo, Naibu wa Rais pia anatarajiwa kupewa baraka na wazee wa jamii ya Wakalenjin.

Licha ya kuzunguka kote nchini tangu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kushirikiana na kinara wa ODM Raila Odinga mnamo 2018, Dkt Ruto ameshikilia kuwa bado hajaanza kampeni.

Kulingana na waandalizi wa hafla ya leo wakiongozwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, jamii ya Bonde la Ufa itamkabidhi rasmi Dkt Ruto kwa Wakenya.

Maelfu ya wafuasi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), wakiwemo zaidi ya wabunge 100, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika mjini Eldoret.

“Mkutano huo ni muhimu kwa sababu wakazi wa Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu, Baringo na Nandi watampa baraka Naibu Rais kumruhusu kuzunguka kila kona ya nchi kusaka kura,” akasema Bw Sudi.

Mbunge huyo alisema kuwa mkutano mwingine utakaojumuisha wakazi wote wa Bonde la Ufa utaandaliwa baadaye katika uwanja wa Afraha, Kaunti ya Nakuru.

“Baada ya mkutano wa Eldoret, tutaandaa mkutano mwingine katika uwanja wa Afraha ambao utaleta pamoja watu wote wa Bonde la Ufa,” akasema Bw Sudi.

Baraka za wazee wa jamii ya Wakalenjin litakuwa pigo kwa Dkt Ruto ni pigo kwa Seneta wa Baringo Gideon Moi ambaye mnamo Februari 2020 alikabidhiwa ‘fimbo ya Nyayo’ iliyokuwa ikitumiwa na baba yake kama ishara ya uongozi.

Baada ya mazishi ya baba yake, Daniel arap Moi, wazee wa jamii ya Wakalenjin walikabidhi Fimbo ya Nyayo kwa mbunge wa Rongai Raymond Moi, ambaye ni kifungua mimba wa Moi.

Baadaye, Raymond alikabidhi fimbo hiyo kwa Gideon Moi ambaye ni kiongozi wa chama cha Kanu. Inahofiwa kuwa Bw Moi ambaye tayari ametangaza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, huenda akagawanya kura za eneo la Bonde la Ufa.

Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago alisema kuwa mkutano wa leo, utakuwa uzinduzi rasmi wa kampeni za Dkt Ruto.

Naibu wa Rais tayari ameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa anazuia wapinzani wake wakiongozwa na Bw Moi, kugawa kura za Bonde la Ufa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Ameagiza wandani wake kuendesha kampeni kabambe kila eneo la Bonde la Ufa kuhimiza wakazi kuunga mkono Dkt Ruto.

Baada ya kupewa baraka za wazee, Dkt Ruto anatarajiwa kukita kambi katika Kaunti za Kericho na Bomet, Jumatatu.

Dkt Ruto tayari ametangaza kuwa wabunge ‘waasi’ wakiongozwa na Joshua Kutuny (Cherang’any), Sila Tiren (Moiben), Dkt Swarup Mishra (Kesses), Seneta Prof Margaret Kamar na Gavana Elgeyo Marakwet Alex Tolgos waadhibiwe kwa kunyimwa kura katika uchaguzi ujao.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Serikali ikomeshe hii hadaa ya...

Waliopewa zabuni ya kufufua Mumias hatarini kutupwa jela

T L