Habari

Wazee kupata matunzo ya kipekee mswada wa Gathoni Wa Muchomba ukipita

July 27th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKONGWE wanastahili kulindwa kutokana na masaibu mengi wanayopitia wakati wa uzee wao.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Bi Gathoni Wa Muchomba, amesema tayari amewasilisha mswada bungeni wa Help Age Bill ama Wa Muchomba Geriatric Bill 2019 ambao itahakikisha wazee wanapata matunzo kwa njia ya kipekee.

Alitoa mfano katika hospitali za nchini akisema ni aibu kwa mkongwe kuwekwa pamoja na mgonjwa wa rika la mwanawe au hata mjukuu kwenye kitanda kimoja.

“Kungekuwepo mpango mwafaka, basi wakongwe wangekuwa wakitengewa mahali spesheli ili wahudumiwe huko na wauguzi wenye ujuzi ya kuwalea vyema,” alisema Bi Wa Muchomba mnamo Ijumaa.

Alizidi kueleza jinsi wakongwe wa kike hudhulumiwa vijijini na vijana; mengi ya matukio hayo yakikosa kutolewa hadharani.

“Kwa hivyo, mswada niliowasilisha bungeni unapendekeza pia wakongwe wajengewe vituo spesheli ambako watapelekwa huko mchana ili wapate maangalizi na matunzo mema,” alisema kiongozi huyo.

Alieleza kwamba mswada huo aliowasilisha bungeni umefika kiwango muhimu cha kujadiliwa ambapo wabunge wengi wameridhishwa na mapendekezo hayo.

Alisema baada ya kuzunguka kote nchini alipata ya kwamba wakongwe wengi wanapitia masaibu mengi ya kiafya na kiakili; na ndiyo maana alilazimika kuja na mapendekezo ya mswada huo.

Ukipita, wakongwe watakaohusishwa ni wa kutoka umri wa miaka 65 hadi zaidi.

Umri

Alizidi kutaja kuwa ni aibu pia kupata mzee wa umri mkubwa akirundikwa pamoja na vijana katika seli ya polisi bila kutambua umuhimu wa umri wake.

Alipendekeza wakongwe wetu wa hapa nchini wapewe huduma bora kama vile wale wa nchi za nje hupokea.

“Afya ya mtu mkongwe yafaa kulindwa kwa hali ya heshima kubwa ili aweze kuongezea siku zake zaidi hapa ulimwenguni,” alifafanua Bi Wa Muchomba.

Kiongozi huyo alikuwa ameandamana na daktari spesheli wa wakongwe, Geriatric Doctor, Dkt Muthoni Gichu aliyesema kuna haja kubwa ya kuwalea wakongwe kwa njia ya weledi.

“Wakongwe ni watu ambao ni rahisi miili yao kupata udhaifu kila mara na kwa hivyo wanahitaji uangalizi wa karibu kila mara,” alisema Dkt Gichu.

Alipendekeza serikali kuwapa mafunzo na kuwaajiri wataalamu watakaojihusisha na malezi ya wakongwe ili kuwapa malezi ya karibu kwa kufuatilia afya yao.