Wazee Mlimani waapa kuleta Kenya pamoja

Wazee Mlimani waapa kuleta Kenya pamoja

NA JAMES MURIMI

WAZEE wa jamii ya Agikuyu wameahidi kuunganisha nchi na kukataa kugawanywa katika mirengo ya kisiasa.

Wazee hao kutoka eneo la Kati wamekubaliana kuunga serikali ya Rais William Ruto itekeleze maendeleo.

Katika uchaguzi wa Agosti, wazee hao waligawanyika kati ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaoongozwa na Raila Odinga na Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto.

Mnamo Ijumaa, mlezi wa kitaifa wa baraza la wazee wa eneo la Kati Kapteni mstaafu Kung’u Muigai, aliitisha mkutano wa maombi katika madhabahu ya Kikuyu iliyoko Naromoru ndani ya msitu wa Mlima Kenya.

Akizungumza na Taifa Leo katika hafla hiyo, Bw Muigai alisema kwamba wanachama wa baraza hilo wameamua kuungana na kuhubiri amani.

“Tumeungana kama wazee wa Agikuyu na tumeahidi hatutagawanywa kwa mirengo ya kisiasa. Kampeni za siasa zimepita na sote tuliibuka washindi kama watu,” alisema.

“Kama wazee, tutakuwa mstari wa mbele kuhubiri amani na umoja ili tuweze kujenga Kenya yenye nguvu. Tumekubaliana kuunganisha Wakenya wote.”

Wazee hao walifanya maombi ya kushukuru Mungu kwa amani iliyoshuhudiwa nchini kabla, kwenye na baada ya uchaguzi wa Agosti.

“Kama wazee kutoka eneo hili, tumefanya maombi ya kutoa shukrani kwa amani ambayo Mungu amejalia nchi yetu baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali. Hatuwezi kuchukulia kwa mzaha amani tunayofurahia kama nchi,” alisema Bw Muigai.

Bw Muigai alisema pia walifanya maombi kuhusiana na ukame unaokumba sehemu za nchi uweze kuisha.

“Kuna sehemu za nchi ambazo zinashuhudia ukame mkali tunaomba Mungu atupe mvua ili tuweze kupata chakula cha kutosha,” alisema.

“Tumeombea watoto wetu wanaoenda shule wanaporudi kwa masomo wiki zijazo ili waweze kufanya vyema.”

Vile vile, waliombea serikali ya Rais William Ruto ili iweze kuongoza nchi kufikia ustawi.

“Kwa wale walioshinda uchaguzi, wakati wa kusherehekea umeisha. Na kwa wale walioshindwa, ni wakati wa kusonga mbele na kujenga nchi. Tunaombea nchi na mambo mazuri yatatoka kwa maombi hayo,” alisema.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti, Bw Muigai, jamaa wa karibu wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta – alikutana na wazee 1,500 wa Kikuyu kutoka eneo la Mlima Kenya katika uwanja wa Kabiruini kaunti ya Nyeri.

Wazee hao walitoka kaunti za Nyeri, Kirinyaga, Murang’a na Laikipia.Katika mkutano huo, Bw Muigai alitangaza kuwa alikuwa na haki ya kuunga mkono mrengo wa kisiasa aliopenda kama vile Bw Uhuru aliyesema alikuwa na haki hiyo.

Hata hivyo, Bw Muigai alisema kwamba familia ilikuwa imeungana licha ya tofauti za kisiasa kati yake na Uhuru.

“Tumeungana kama familia ya Kenyatta. Juzi tulikutana nyumbani kwa harusi ya kitamaduni. Lakini tukitoka nje ya lango, sisi ni Wakenya,” Bw Muigai alisema.

  • Tags

You can share this post!

Maonyesho ya kimataifa ya vitabu yarejea baada ya kutatizwa...

Barasa aamrisha idara ya afya idhibiti ebola

T L