Habari Mseto

Wazee mnaovuta bangi mnachangia vijana kupotoka – kamishna

October 21st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya wazee kuwa kielelezo kwa vijana ili waweze kuiga mfano wao.

Hayo yalitajwa na Naibu Kamishna wa Thika Mashariki Bw Thomas Sankei.

Alisema Jumapili kwamba uchunguzi wake umebainisha ya kwamba katika eneo la Makutano, Kilimambogo, wazee wameonekana wakivuta bangi na hiyo ni ‘tabia mbaya’ mbele ya vijana.

“Nyinyi wazee inaonekana mmevuka mpaka sasa. Badala ya kutoa mfano mwema, nyinyi ndio mnavuta bangi,” alisema Bw Sankei.

Alisema wazazi wana jukumu kubwa la kuwapa vijana mawaidha ili waweze kuwa raia wema wa kutegemewa.

Alisema imefika wakati kila mmoja awe mstari wa mbele kuwaleta vijana karibu na kuwapa mawaidha na mwelekeo ufaao.

“Kila mara tunaposhuhudia mambo mabaya ni sharti tuseme hapana kwa sauti ya juu. Vijana hawa walio mbele yenu wanataka kusikia mengi kutoka kwenu,” alisema Bw Sankei.

Alisema vijana wamejaliwa vipaji tofauti na kwa hivyo wanastahili kuvitumia vilivyo kwa sababu ndivyo vitawainua katika maisha ya baadaye.

“Nimefurahishwa na vipaji vya vijana hawa na iwapo watakuza talanta hizo, bila shaka watafanikiwa katika siku zijazo,” alisema afisa huyo mkuu.

Aliyasema hayo wakati wa sherehe za Mashujaa Dei ambazo katika Kaunti ya Kiambu zilifanyika katika mkao makuu ya naibu wa Kamishna eneo la Kilimambogo.

Aliwataka wakazi wa eneo la Kilimambogo na maeneo jirani wawe na umoja na washirikiane kwa jambo lolote lile.

Alisema umoja ndiyo nguvu kwa umma.

Mabadiliko kadhaa

Mwakilishi wa naibu gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, Bw Peter Kang’ethe alisoma hotuba ya kaimu gavana huku kukiwa na mikakati ya kuleta mabadiliko kadhaa katika Kaunti hiyo.

Kulingana na mipango hiyo, Kaunti ya Kiambu iko tayari kufanya kazi kwa pamoja na serikali kuu.

Mipango hiyo inaelezea wamiliki wote wa baa za kuuza pombe watabuni vyama vya ushirika kama njia mojawapo ya kujiendeleza na kuwa pamoja.

Alieleza ya kwamba hospitali zote – kuanzia kiwango cha Level 5 hadi Level 2 zitapata dawa bila kukosa na hii inatokana na kampuni ya kusambaza dawa ya Kemsa kutoa hakikisho kuwa dawa zitapatikana.

Alisema sekta za chai na kahawa zinafanyiwa uangalizi mpya ili kuziboresha zaidi.

Ripoti ya naibu gavana ambaye kwa sasa ndiye kaimu gavana wakati Gavana Waititu akikabiliwa na kesi mahakamani, ilidai ya kwamba kwa muda mrefu kumekuwa na usimamizi mbaya wa sekta hizo mbili na kwa hivyo, ni sharti jambo la dharura lifanywe.

Alikariri ya kwamba kila mfanyakazi atapewa nafasi yake kutekeleza wajibu wake bila kutishwa na yeyote.