Habari Mseto

Wazee Rift Valley wataka ‘deni’ lilipwe

June 28th, 2019 2 min read

Na OSCAR KAKAI na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wazee wa jamii ya Kalenjin, hatimaye wamewataka wenzao wa Agikuyu kuheshimu ahadi waliyotoa kwa Naibu Rais William Ruto.

Akiongea na wanahabari mjini Kapenguria, mwenyekiti wa baraza la wazee la jamii hiyo tawi la Pokot Magharibi James Lukwo aliwataka wenzao wa jamii ya Agikuyu kuheshimu ahadi hiyo akisema ndiyo ilichangia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.

“Tunakubali kuwa jamii ya Agikuyu haina deni la kisiasa kwa jamii yetu ya Kalenjin kwa sababu hamna mkataba ambao ulitiwa saini baina ya jamii hizi mbili. Hata hivyo, tunafahamu kuwa kuna ahadi ambayo Rais Kenyatta alitoa hadharani kwamba atamuunga mkono naibu wake Dkt Ruto baada ya kukamilisha kipindi chake cha uongozi 2022. Hii ndiyo ahadi ambayo tunaomba wenzetu wa Agikuyu waheshimu,” alisema Mzee Lukwo.

“Hata Naibu Rais mwenyewe amefafanua kuwa hakuna deni la kisiasa ambalo anadai mtu yeyote. Lakini amekariri kuwa atawania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao. Hii ndiyo maana tunaomba ndugu zetu wa Agikuyu kumuunga mkono kama njia ya kuendeleza uhusiano mzuri kati ya jamii hizi mbili,” Mzee Lukwo aliongeza.

Bw Lukwo, ambaye alikuwa ameandamana na wenzake aliwataka wazee wa Agikuyu kukoma kumkashifu Dkt Ruto na badala yake watoe nafasi kwake na Rais Kenyatta ili waweze kutimiza ahadi yao kwa Wakenya, hasa katika nyanja za maendeleo.

“Uhusiano kati ya Rais na naibu wake bado ungali imara. Kwa hivyo, sote twapaswa kuwapa nafasi ya kuwatumikia Wakenya jinsi walivyoahidi. Hizi propaganda zinazoendeshwa kwamba viongozi hawa wawili hawaelewani hazina mashiko na zinafaa kupuuzwa,” alieleza.

Kampeni

Kauli ya wazee hao inajiri siku chache baada ya wenzao wa Agikuyu kumtaka Dkt Ruto kumheshimu Rais Kenyatta kwa kukomesha kampeni za mapema huku wakikariri kuwa hawana deni la kisiasa kwa mtu yeyote.

Aidha, kuchipuka kwa mgwanyiko ndani ya chama tawala cha Jubilee baada ya kubuniwa kwa makundi mawili yenye misimamo kinzani kuhusu azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022, kumepalilia dhana kuwa huenda Rais Kenyatta akaunga mkono mtu mwingine kuwa mrithi wake.