Habari Mseto

Wazee wa Agikuyu sasa wapanga kusimamia tohara

November 12th, 2019 1 min read

Na WAIKWA MAINA

BARAZA la Wazee wa jamii ya Agikuyu limefutilia mbali sherehe na hafla zake zote hadi Januari ili kuchukua usukani wa tohara ya wavulana msimu huu.

Hatua hii imekusudia kuzuia marudio ya visa vya kutisha vilivyotokea mwaka uliopita.

Wakizungumza katika Shule ya Msingi ya Kagai iliyo Tumaini, Kaunti ya Nyandarua, viongozi wa baraza hilo walitangaza uamuzi wao wakisema wanataka kuyapa umuhimu maslahi ya mtoto mvulana.

Walikuwa wamehudhuria hafla ambapo Gavana wa Nyandarua, Bw Francis Kimemia alitawazwa kuwa mzee wa jamii.

Wazee hao walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Utamaduni cha Wakikuyu, Bw Ndung’u Gaithuma, waliomba wazazi kupeleka watoto wao kwa tohara katika maeneo ambapo wana hakika watapewa ushauri na elimu bora kuhusu tamaduni zao.

“Tunaomba pia kina baba waruhusu wana wao wawe wakiwaandama kila wanakoenda ili wapate muda wa kutosha kuwafunza kuhusu majukumu ya mwanamume katika jamii,’ akasema Bw Gaithuma.

Mwaka uliopita, kulikuwa na visa vya wavulana kuteswa katika maeneo yote ya jamii hiyo wakati walipopelekwa kupashwa tohara.

Baadhi ya wavulana walipigwa hadi wakafariki ikidaiwa walikuwa wanafunzwa kuwa jasiri inavyotakikana kwa wanaume, mikononi mwa makundi ya kihalifu yaliyojifanya kuwa washauri wa kijamii.

Magenge hayo yalikashifiwa pia kwa kuwapa wavulana mafunzo ya itikadi kali za kijamii na kuwaingiza katika makundi ya kihalifu ambayo wanachama huwa ni waraibu wa mihadarati ikiwemo bangi.

Kuna wavulana wengine ambao walipata majeraha ya kudumu maishani, na baadhi wakalazwa hospitalini kwa muda mrefu kuuguza majeraha yao ya kimwili na kisaikolojia.