Habari MsetoSiasa

Wazee wa Agikuyu wamkataa Ngunjiri kuwa msemaji wa jamii

July 23rd, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

Mzozo unatokota baada ya Baraza la wazee la Agikuyu kusema halitamtambua mbunge wa Bahati Kimani Nginjiri, kama msemaji wa jamii hiyo eneo la Rift Valley.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao eneo hilo James Nene na aliyekuwa mbunge wa Njoro Joseph Kiuna, wazee hao walimpuuza Bw Ngunjiri kama mtu anayejitafutia sifa ambaye anataka kuzua uhasama kati ya jamii za eneo hilo.

“Tunakataa hatua zote za kutulazimishia Bw Ngunjiri au mtu yeyote kuwa msemaji wa jamii eneo hili,” wazee hao walisema kwenye taarifa iliyosomwa na mwenyekiti James Nene.

Wazee hao walisisitiza kuwa walikubaliana msemaji wa jamii ni Rais Uhuru Kenyatta.

Walisema hawatambui wadhifa uliobuniwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Bw Ngunjiri nyumbani kwake Bahati mnamo Jumamosi.

Jana, walilaumu viongozi wa jamii kutoka eneo la Kati ya Kenya kwa kuingilia uongozi wa Rift Valley.

“Huu ni mwelekeo mbaya na ni sawa na kutengwa kwa jamii moja na ndugu zao,” ilisema taarifa ya Nene.

Walisema kuna njama za kugawanya jamii hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Wazee waliokutana nyumbani kwa Bw Ngunjiri sio wazee halali wa jamii ya Agikuyu na ndio sababu tunakataa maazimio yao,” alisema Bw Nene.

Mwenyekiti wa kitaifa wa baraza hilo, Bw Ndungu Gaithuma, alisema ni makosa kwa Bw Ngunjiri kujitawaza msemaji wa jamii hiyo ili kutimiza maslahi yake ya kibinafsi.

“Mkutano katika boma la Bw Ngunjiri ulikuwa wa kula mbuzi na haufai kutumiwa kuchagua kiongozi wa jamii,” alisema Bw Gaithuma.

Kwingineko, wanafunzi wa chuo cha Mount Kenya waliandamana hadi kituo cha Polisi cha Thika kulalamikia mwenzao aliyeuawa na majambazi. Wakiongozwa na Kevin Theuri, walifululiza hadi katika afisi ya OCS wa Thika Bw Mathew Masanga aliyefanya kikao nao kwa muda wa dakika 30. Walidai kuwa mnamo Alhamisi mwanafunzi wa mwaka wa tatu alidungwa kisu na wahalifu waliompora simu yake huku wakimwacha hoi.

Mwanafunzi huyo alipatikana ameaga dunia na wapita njia ambao walipiga ripoti kituo cha polisi, ambao walimpeleka hifadhi ya maiti ya Thika Level 5.

Ripoti za Francis Mureithi, Peter Mburu na Lawrence Ongaro