Habari

Wazee wa Gema wamkaidi Uhuru

July 23rd, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAZEE wa jamii za Gikuyu, Embu na Meru (Gema), wamepinga mpango wa kuvunja muungano huo na nafasi yake kuchukuliwa na baraza jipya la Wazee wa Mlima Kenya (MKCE).

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa mpango huo wa kubuni MKCE unasukumwa na wandani wa Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi za kuhakikisha ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu hatima ya kisiasa ya eneo hilo.

Mwenyekiti wa Gema, Askofu Mstaafu Lawi Imathiu aliambia Taifa Leo kuwa hatua hiyo inasukumwa kwa maslahi ya kibinafsi wala sio kwa manufaa ya jamii hizo.

Askofu huyo alisema hakuna yeyote ambaye ana ukiritimba wa kuamulia watu jinsi ya kufanya maamuzi yao ya kisiasa, mbali hilo ni jukumu la wenyeji.

Hofu ya Askofu Imathiu ni kuwa mabadiliko hayo yanasukumwa kwa lengo la kuwazima wengine kuwa na usemi wa hali ya baadaye kisiasa ya Mlima Kenya.

Hii imezuka kukiwa na mivutano ya kimaeneo kuhusu anayepasa kumrithi Rais Kenyatta kama msemaji wa eneo hilo kisiasa, duru zikisema kiongozi wa nchi anapendelea aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.

Hatua hiyo imeonekana kutofurahisha jamii ya Ameru, ambao wanajihisi wakati umefika kwa mmoja wao kuungwa mkono na Agikuyu kama “mfalme” wa Mlima Kenya.

“Msimamo wa Gema kwa sasa ni kuwa yeyote ambaye anajihisi kuwa anaweza kuwa kiongozi wa eneo hili ajitokeze, kisha sisi tutawapiga darubini na kwa kuhusisha watu wote wa Mlima Kenya tuamue ni nani anayefaa zaidi,” akasema Askofu Imathiu.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu, Wachira Kiago alitaja mpango huo kuwa unaosukumwa na watu wachache kwa ajili ya kuafikia malengo yao ya kisiasa.

Kwa Mujibu wa aliyekuwa mkuu wa mkoa Joseph Kaguthi, kuna baadhi ya watu ambao hawako tayari kukumbatia maoni tofauti na yao.

“Kuna mtu ambaye anapotosha wanasiasa wa Jubilee kuwa kusambaratisha kila muungano au mrengo ambao uko na maoni tofauti ya kisiasa ni kujenga nchi,” akasema Bw Kaguthi.

Maoni hayo yaliungwa mkono na Katibu wa muungano wa Mihiriga Kenda katika Kaunti ya Kirinyaga, Nahashon Kabeu aliyesema: “Kuna kundi la watu ambalo linalenga kuvunja umoja wa Gema kwa upotovu kuwa linamjenga Rais Kenyatta, ilhali linambomoa.”

Habari zinaeleza kuwa mpango wa kuvunja Gema na mahala pake kuchukuliwa na MKCE unalenga kuwiana na ajenda ya Rais Kenyatta ya kuunganisha eneo la Mlima Kenya chini yake.

Hatua hiyo, duru zilieleza, zitampa Rais Kenyatta uwezo wa kubakia kuwa mwenye ushawishi mkuu wa kisiasa eneo la Mlima Kenya ili kumpa nafasi ya kutoa mwelekeo wa urithi wa urais katika kura ya 2022, na pia kuamlia eneo hilo msemaji.

Askofu Imathiu alisema kwa sasa haja kuu ya wakazi wa Mlima Kenya ni maendeleo na kukabiliana na umaskini, wala sio maandalizi ya siasa za urithi wa 2022.

Alieleza kuwa eneo hilo halifai kufungia nje mtu yeyote kwa kuwa ni katika kuwakubalia wote kujieleza waziwazi kwa raia, ambapo aliye na maono bora zaidi kuhusu maendeleo ya eneo hilo atapatikana.

Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe ametetea hatua hiyo akisema Rais yuko mbioni kurejesha sauti yake katika Mlima Kenya.

“Rais Kenyatta alichaguliwa na wenyeji wa Mlima Kenya kuwaakilisha katika siasa za eneo na pia katika serikali. Ni kinaya kikubwa kuwa wale ambao hawakuchaguliwa na raia kutekeleza wajibu huo wanajifanya ndio wa kuwakilisha eneo hili kisiasa,” akasema Bw Murathe.

Naye Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata aliambia Taifa Leo kuwa harakati za Rais zinalenga kuhakikisha eneo la Mlima Kenya lina umoja wa kisiasa.