Wazee wa Kaya mbioni kuunganisha Wapwani

Wazee wa Kaya mbioni kuunganisha Wapwani

Na MAUREEN ONGALA

WAZEE wa jamii za Wamijikenda sasa wamejitwika jukumu la kuongoza juhudi za kuleta umoja wa kisiasa Pwani, baada ya wanasiasa kuonekana kulemewa.

Wazee hao wa Kaya wamesema migawanyiko ya wanasiasa katika mirengo tofauti inaendelea kuathiri maendeleo katika ukanda huo, na kwamba wanahitaji kuungana kabla uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika kituo cha utamaduni cha Magarini, Kaunti ya Kilifi, mratibu wa Muungano wa Wazee wa Kaya za Mijikenda, Bw Tsuma Nzai, alisema tayari washaanza kufanya mikutano kujadili mikakati watakayotumia kuleta pamoja wanasiasa wa eneo hilo.

Alisema mojawapo ya maamuzi yaliyofanywa kwa sasa ni kuwa, wazee wa kijamii wanaotambuliwa na muungano huo ndio pekee watakubaliwa kutangaza wanasiasa ambao wanastahili kuungwa mkono na jamii.

“Hakuna mzee mwingine yeyote wa Kaya atakubaliwa kupeana baraka kwa wanasiasa isipokuwa wale watakaoidhinishwa na baraza,’ alieleza.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, amekuwa mstari wa mbele kupigania umoja wa Wapwani kuelekea kura 2022.

Hata hivyo, mpango huo haujapokewa vyema na viongozi wengi ambao wametengana kwa mirengo mbalimbali; hasa miwili inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto na ule wa Kinara wa ODM Raila Odinga.

Hivi majuzi, ilibainika kuwa vyama vitano ambavyo awali vilitarajiwa kuvunjwa ili kuunda chama kimoja cha Pwani, viliamua vitaunda muungano mbadala.Vyama hivyo ni Kadu-Asili, Shirikisho, Communist Party of Kenya (CPK), Umoja Summit Party of Kenya na Republican Congress Party.

“Iwapo wanasiasa watakataa kutambua ushauri wa wazee kutimiza malengo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, wakumbuke kuwa lengo letu sisi huwa kutakia jamii mema,” alihoji Bw Nzai.

Msimamo huo uliungwa mkono na Mzee Kenya Mbeo kutoka Kaya Kambe. Alisema: “Azimio letu ni kuona jamii zote za Pwani zikiungana na kuzungumza kwa sauti moja kisiasa. Hiyo ndiyo njia pekee itakayotuwezesha kutimiza malengo yetu ya kimaendeleo. Bado tuko katika lindi la umasikini kwa sababu hatuna msiamamo mmoja wa kisiasa.”

Katibu Mkuu wa Chama cha Umoja Summit, Bi Naomi Cidi, alisema wazee wamekuwa wakihusishwa katika mazungumzo ya kutafuta umoja wa kisiasa Pwani, akisisitiza kuwa misimamo yao iheshimiwe na wanasiasa wote.

Alisema wataendelea kushirikiana na wazee kubaini makosa ya miaka ya nyuma ili yaepukwe.

  • Tags

You can share this post!

Beki Ben White aingia Arsenal kuchukua nafasi ya David Luiz

Ruto akatwa mbawa