Wazee wa Kaya sasa wavuruga karata za Jumwa

Wazee wa Kaya sasa wavuruga karata za Jumwa

Na MAUREEN ONGALA

WAZEE wa Kaya wamezamia siasa za urithi wa kiti cha ugavana Kaunti ya Kilifi, katika hali ambayo itavuruga hesabu za wanasiasa wengi wanaomezea mate kiti hicho mwaka ujao.

Huku wakimtawaza Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi kurithi kiti hicho, walipitisha uamuzi kuwa kiti hicho kinafaa kuzunguka kutoka kwa kabila moja hadi nyingine.

Kwa msingi huu, uamuzi wao ni kuwa gavana anayefaa kuingia wakati Bw Amason Kingi atakapomaliza kipindi chake cha uongozi, hafai kutoka kwa jamii ya Wagiriama.

Bw Saburi hutoka katika jamii ya Warabai.Idadi kubwa ya viongozi wanaopanga kuwania kiti hicho kufikia sasa ni Wagiriama, akiwemo Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Mbunge wa Magarini Michael Kingi na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi Gideon Mung’aro.

Bw Saburi wiki iliyopita alitangaza rasmi azimio lake kutumia chama cha ODM kwa kinyang’anyiro hicho.

Mratibu wa Chama cha Wazee wa Kaya za Mijikenda, Bw Tsuma Nzai alisema wakati umefika kwa jamii ya Wagiriama kuunga mkono Mrabai kwa wadhifa huo.

“Tunawapongeza Warabai kwa kuunga mkono jamii ya Wagiriama kuongoza kaunti kwa vipindi viwili na tuna hakika wao pia wana viongozi bora. Sasa ni wakati wa Wagiriama kurudisha shukrani na kumkubali naibu gavana wetu aongoze Kilifi,” akasema.

Bw Nzai alisema wazee waliamua kiti hicho si mali ya jamii moja pekee bali kinafaa kushikiliwa na kila kabila katika jamii.

Waliongeza kuwa wameamua kumuunga mkono Bw Saburi kwa vile amekuwa mtiifu kwao kwa miaka mingi na pia amedhihirisha kuwa mwadilifu uongozini.

Walikuwa wameongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazee Wamijikenda, Mzee Mwalimu Mbwisho kutoka Kaya Digo iliyo Kaunti ya Kwale.

“Naibu gavana wetu amekuwa akitusaidia kwa njia zozote zile bila kuchelewa hata anapokuwa na shughuli nyingi kazini. Hii inaonyesha kuwa yeye si mbinafsi na ataongoza jamii vyema,” akasema.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kaya Ribe iliyo Kaunti Ndogo ya Rabai wakati wa kuzindua maombi ya kitamaduni yanayonuiwa kusihi miungu walete mvua, na kukemea kiangazi kilichosababisha ukame na njaa na matatizo mengine katika jamii.

Waliombea pia umoja wa jamii ya Wamijikenda na Pwani nzima kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.? Mzee Mbwisho alisema hatua yao ya kumuunga mkono Bw Saburi ni mwanzo wa kutafuta umoja wa Wamijikenda.

Kulingana naye, umoja wa Pwani unakumbwa na changamoto nyingi kwa sababu ya viongozi wabinafsi ambao wanajali maslahi yao ya kibinafsi.? “Pwani haitapitia matatizo mengi ikiwa jamii ya Wamijikenda itaungana.

Tunaendelea kuwa nyuma kisiasa na kiuchumi kwa sababu hatuna umoja. Tumekubalia viongozi wa nje ya eneo hili kutugawanya kila mara tunapojaribu kuungana,” akasema.

Hali hiyo ndiyo imelaumiwa kusababisha vikwazo kwa juhudi za kuunda chama cha Pwani kabla 2022 ambazo zinaongozwa na Gavana Kingi.

Kwa upande wake, Bw Julius Saha alisema majadiliano kuhusu hitaji la kufanya kiti cha ugavana kiwe kikizunguka kutoka jamii moja hadi nyingine yalianza katika Kayafungo ambayo huwakilisha jamii pana ya Wagiriama.

“Hatua hii italeta umoja kwa jamii ya Wamijikenda. Hatutaki hali ambapo makabila ya watu wachache yataanza kuhisi kama yametengwa uongozini. Kila jamii inafaa kupewa nafasi ya kuongoza,” akasema.

Bw Saburi alitoa wito kwa wazee hao kuwachunguza kwa kina viongozi wote ambao wataenda kwao kutafuta uungwaji mkono.

You can share this post!

UDA kufanya uchaguzi wa mashinani Oktoba – Muthama

Maangi asema atahepa Ruto Matiang’i akiwania