Wazee wa Kaya watakasa barabara

Wazee wa Kaya watakasa barabara

Na MAUREEN ONGALA

USAFIRI kwenye barabara kutoka Malindi–Mombasa ulilemazwa kwa saa kadhaa Ijumaa baada ya wazee wa Kaya wa jamii ya Mijikenda kufunga barabara hiyo kwenye eneo la Kizingo kwa shughuli maalum ya utakaso ili kuzuia visa vya ajali za barabarani.

Eneo la Kizingo limeorodheshwa kama hatari zaidi kufuatia visa kadhaa vya ajali, huku kisa cha hivi majuzi kikiwa ajali mbaya iliyohusisha mabasi mawili yaliyogongana mnamo Aprili 8, na kuwaua watu 15.

Wazee hao waliokusanyika katika eneo ambapo ajali hiyo ilifanyika wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni, walifanya maombi maalum kuwatuliza miungu, wakaomba msamaha na kukemea mikosi inayosababisha ajali hizo za barabarani.

Matambiko hayo maalum yalifanywa na mganga mashuhuri kwa jina Mzee Bimumba Sulubu Nzai kutoka Wadi ya Adu, eneo la Magarini.

Wazee hao walitembea kwenye barabara hiyo wakiwa wamebeba kuku mweusi, jogoo mwekundu, mbuzi pamoja na jungu la kienyeji lililojaa mchanganyiko wa tiba za kiasilia.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mwelekezi wa Muungano wa Wazee wa Kaya wa jamii ya Mijikenda, Tsuma Nzai, alisema ni muhimu kufanya matambiko ili kuokoa maisha dhidi ya kukatizwa kupitia ajali za barabarani katika kaunti hiyo.

Alisema matambiko hayo yalikuwa sehemu ya maombi maalum ya wazee wa Kaa yaliyoanza Ijumaa, wiki iliyopita katika eneo la Kaya Ribe, Rabai.

“Maombi hayo yalipangwa na wazee walioanza kwa maombi maalum katika Kaya Ribe ili kuwaomba miungu kuingilia kati dhidi ya pepo wabaya wanaosababisha ukame, vifo, na maradhi,” alisema.

Mwelekezi huyo alisema kuwa kando na eneo hilo la ajali, matambiko hayo ya utakaso pia hufanyiwa watu waliojitia najisi kwa kuua kwa kutumia bunduki au panga.

Baada ya Kaya Ribe, wazee hao walienda katika kituo cha Kaya Godoma kuwatembelea wazee ambao wametafuta hifadhi katika makao hayo kwa kuhofia kuuawa kuhusiana na madai ya uchawi.

Viongozi hao wataelekea katika kituo cha Mekatilili Menza, Magarini kwenye maeneo matakatifu ya Mipoho na Kaya Kinondo katika Kaunti ya Kwale, ili kupata Baraka kutoka kwa miungu wa kiume na wa kike wa jamii ya Mijikenda.

Bw Nzai alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta na magavana kuendeleza itikadi na tamaduni za jamii mbalimbali ili kuimarisha amani na umoja nchini.

Aliihimiza serikali kushirikiana na kusaidia wazee wa Kaa kama vigogo wa amani nchini.

You can share this post!

Biden aipapura Facebook kutozima habari za uongo kuhusu...

Magoha azuia vyuo vikuu kuongeza karo, mageuzi