Siasa

Wazee wa Kaya watisha kumlaani Jumwa kwa kumtetea Sudi

September 15th, 2020 2 min read

CHARLES LWANGA na MAUREEN ONGALO

WAZEE wa Kaya katika jamii ya Mijikenda wametishia kuwalaani viongozi wa Pwani wanaounga mkono matamshi ya chuki ya mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi na mwenzake wa Emurua Dikirr, Bw Johana Ng’eno ambao wanakabiliwa na mashtaka.

Wazee hao kutoka Kaya tisa za Mijikenda kat?ka Kaunti ya Kilifi, Mombasa na Kwale walisema pia walitishia kuwakataa viongozi hao kuwa mmoja wa jamii yao kwa kuunga mkono matamshi ya chuki kuhusu Rais Uhuru Kenyatta na mamake Ngina Kenyatta.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kaya, Bw Stanley Kenga kutoka Kaya ya Ribe, walisema wamesikitishwa na baadhi ya viongozi waliochaguliwa na watu kwa kuelekeza nchi upande mbaya wenye matusi.

“Tumeshangazwa na mwenendo huu na inasikitisha kuona vijana hawaheshimu kiongozi wa nchi na mamake. Twafaa tuheshimu viongozi wetu jinsi viongozi wetu -kina Gavana Amason Kingi wa Kilifi, Gavana Hassan Joho (Mombasa), na wa Kwale Salim Mvurya wanavyofanya,” alisema.

Mzee huyo alisema kuwa kwa pamoja wametangaza laana kwa wabunge wawili hao pamoja na wote wanaomtetea.

Haya yanajiri siku moja baada ya viongozi wa Pwani katika mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao ni marafiki wa kiasiasa wa Naibu Rais William Ruto, kutetea matamshi ya Bw Sudi na Ng’eno, akiwemo aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar na mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa ambaye alisafiri hadi mahakama ya Nakuru mnamo Jumatatu iliyopita kuonyesha umoja na wabunge hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kueneza jumbe za chuki.

Jana, wazee wa Kaya walisema wanawalaani vikali wabunge hao na wakataka wajiuzulu uongozini kwa kukosa hekima, unyenyekevu na heshima kwa Rais Kenyatta na mama yake.

“Ikiwa serikali haitawachukulia hatua, tutachukua jukumu la kuwapa mwelekeo. Historia ya Kenya inatokea zama za mwanzilishi wa nchi hii hayati Jomo Kenyatta ambaye alitembelea wazee wa Kaya kwa mawaidha na kutuonyesha heshima,” alisema.

Bw Hamisi Juma Mwaviko, mmoja wa wazee wa Kaya kutoka Digo, alisema wamesikitishwa kwa matusi yaliyoelekezwa kwa mamake Rais kwa sababu mama wa mtu mwengine ni kama mama yao.

“Wao watahisije ikiwa mama yao atatusiwa? Matamshi hayo yanahuzunisha na ni laana. Ni kiongozi wa aina gani haheshimu viongozi, kwani huko katika jamii yao hakuna wazee wanaoweza kumfundisha heshima? Hapa Pwani tunajua hao viongozi kwa majina na tutawaalika siku nyingine kuwakashifu.”

Bw Mwaviko alisema mama yake Rais ambaye pia ni mama wa kwanza wa taifa si mwanasiasa wala hataki kiti cha udiwani, ubunge wala ugavana, hivyo basi hafai kutukanwa au kuhusishwa na siasa chafu za wabunge hao.

Kwa upande wake, Bw Tsuma Nzai Kombe ambaye ni mpangaji maalum wa baraza la wazee wa kaya la Mijikenda alimtaka spika wa bunge, Bw Justin Muturi aingilie kati na ‘kusafisha’ nyumba yake bungeni ikiwemo kuwaadhibu wabunge wapotovu.

“Ingawaje viongozi wanazungumza kwa niamba ya jamii, wanafaa wawe makini na matamshi yao ili wasilete chuki,” alisema.

na kuongeza “tume ya maridhiano na utengamano (NCIC) inafaa iambie wakenya ni hatua gani wamechukuwa kutatua swala hili kwa sababu tunaelekea uchaguzi mkuu ili kuzua vita vya uchaguzi kama zile za 2017.”

Vile vile, alitaka vyama vya siasa na wazee wa jamii watoe misimamo yao kuhusiana na matamshi hayo ya wabunge na kukashifu vikali matamshi ya viongozi ambao wanaeleza chuki.