Habari Mseto

Wazee wa mitaa sasa wanusia ajira rasmi serikalini

May 13th, 2024 1 min read

NA KITAVI MUTUA

ZAIDI ya wazee wa mitaa 45,000 huenda wakaajiriwa hivi karibuni baada ya serikali kualika maoni kutoka kwa Wakenya kuhusu uwezekano wa kuwapatia majukumu rasmi.

Hii inafuatia kukubalika kwa Mswada wa Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ambao unataka wazee wa mitaa watambuliwe rasmi.

Mswada huo wa Mutuse ulipendekeza kubadilisha Sehemu ya 14 ya Sheria ya Ushirikishi wa Kitaifa kupanua mfumo wa utawala kujumuisha wazee wa mitaa.

Mbunge huyo ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya Kisheria, anasema kwamba wazee wa mitaa wamekuwemo tangu uhuru wakitoa huduma muhimu kwa serikali bila malipo, kinyume na Kipengele cha 41 cha Katiba kuhusu haki katika ulipwaji kwa kazi iliyofanyika.

Kwenye Mswada huo, Bw Mutuse alikuwa amependekeza kwamba kila mmoja wa zaidi ya wazee hao 45,000 alipwe kati ya Sh7,000 na Sh12,445 kwa mwezi kwa majukumu yao ya kusimamia masuala ya kiutawala nyanjani.

Kulingana na notisi ya kutoa maoni iliyotolewa na Katibu wa Wizara ya Ndani Raymond Omollo, Wakenya wana hadi Juni 6 kutoa maoni yao kwa maandishi kuhusu pendekezo la sheria hiyo.

Miongoni mwa masuala ya kuamuliwa ni uhitimu wa kimasomo, uajiri na umri wa kustaafu wa wazee wa mitaa pamoja na majukumu kamili na malipo.

Kumekuwa na makubaliano kwamba wasivalishwe sare kama machifu na manaibu chifu.

Bw Mutuse anasema alichochewa na mahangaiko ya wazee wa mitaa wanapoendelea kutekeleza majukumu yao kwa serikali ya kitaifa bila malipo yoyote na kwamba anaonelea watafanya makuu iwapo watalipwa.