HabariSiasa

Wazee wa Mulembe wamruka Mariga

September 23rd, 2019 2 min read

JOHN ASHIHUNDU na VALENTINE OBARA

MGOMBEAJI ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra kwa tikiti ya Chama cha Jubilee, Bw McDonald Mariga amepata pigo baada ya kikundi cha wazee wa jamii ya Waluhya, kuamua kutomuunga mkono.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wamekuwa wakisema kuwa Bw Mariga, anayeaminika kupendekezwa na Naibu Rais William Ruto, alitarajia kuvutia idadi kubwa ya wanajamii hiyo wanaoishi Kibra ili kupata ushindi.

Katika uchaguzi huo mdogo uliotokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge Ken Okoth, wagombeaji wengine wanaotoka katika jamii ya Waluhya (Mulembe) ni Bw Khamisi Butichi wa chama cha Ford Kenya na Martin Andati wa chama cha Modern Alliance Party.

Hata hivyo, chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, aliye mmoja wa vigogo wa kisiasa wa jamii hiyo ya Magharibi, kinamdhamini Bw Eliud Owalo ambaye si wa kutoka katika jamii hiyo.

Kama ilivyo desturi ya siasa za Kenya, wakati mwingi kura hupigwa kwa misingi ya kikabila. Ni kwa msingi huu ambapo huenda msimamo wa wazee hao ukashawishi kwa kiwango fulani msimamo utakaochukuliwa na jamii ya Waluhya ambao watapiga kura Kibra.

Wazee hao wanaosemekana kuwa na ushawishi kwa masuala ya jamii ya Waluhya ambao walizungumza jana katika Kaunti ya Nairobi, walisema walitumia mbinu maalumu kuchagua kati ya ‘wana wao’ watatu.

Bw Butichi aliibuka mshindi kwa kupata alama 470 chini ya 700 na kuwashinda Bw Andati na Bw Mariga walipata alama 430 na 385 mtawalia.

Akitangaza matokeo hayo jana katika ukumbi wa Railway Cub, mwenykiti wa baraza hilo linalojitambua kama Obulala Unity of Purpose, Bw Richard Ekhalie alisema jamii ya Waluhya ndio ina idadi kubwa eneo la Kibra.

“Miongoni mwa mbinu tulizotumia kupata mshindi ni pamoja na uwezo wa kifedha, ujuzi wa uongozi, umaarufu, ajenda zake kwa watu wa Kibra, kabila pamoja na mahojiano ya moja kwa moja na wakazi wa Kibra,” akasema Bw Ekhalie.

Bw Ekhalie alisema kundi lao ambalo lilibuniwa 2014 sio la kisasa, mbali la kuangalia maslahi ya Waluhya kwa jumla.

“Tulipewa jukumu na watu wa jamii ya Mulembe kuwapa mgombeaji mmoja. Tulifanya mahojiano ya moja kwa moja na wagomeaji wote kutoka jamii ya Mluhya ambapo Butichi aliibuka mshindi,” akasema Bw Ekhalie.

Wengine waliokuwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na Vincent Shimoli, Jeremiah Imbali, Suma Musine na Moses Wanani.

Hata hivyo, Bw Mariga anatarajiwa kupata ushindani mkali zaidi kutoka kwa Benard ‘Imran’ Okoth wa ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga.

Wiki iliyopita, baadhi ya viongozi wa eneo la Magharibi waliwalaumu Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kwa kusimamisha wagombeaji Kibra ilhali wao hudai wanatetea umoja wa Waluhya.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepanga uchaguzi huo kufanyika Novemba 7.