Habari Mseto

Wazee waficha mvi wasiuawe

July 30th, 2019 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAZEE eneo la Pwani wanalazimika kuvaa kofia kukuficha mvi wakihofia kuuawa. Pia wengi wameanza kupaka rangi nyeusi nywele zao wasije wakatambuliwa kuwa wana mvi.

Kwa muda sasa, magenge yamekuwa yakitekeleza mauaji ya kinyama ya wazee wenye mvi kwa kisingizio kuwa ni wachawi.

Kulingana na Mshirikishi wa Serikali Kuu eneo la Pwani, Bw John Elungata, wazee hao wameingiwa na hofu, ndiposa wameamua wawe wakivaa kofia ili kuficha nywele hizo, ambazo badala ya kuwa ishara ya busara zinawaweka kwenye hatari ya kuuawa.

Bw Elungata aliwaonya wakazi dhidi ya kuwauawa wazee hao kwa visingizio kuwa ni wachawi, lakini lengo kuu likiwa ni kuchukua mashamba yao.

“Wazee wanaficha nywele nyeupe kwa kuvaa kofia. Kuna sehemu fulani hapa ukionekana na nywele nyeupe uko hatarini,” akasema Bw Elungata.

Kulingana na mshirikishi huyo, wazee katika Kaunti ya Kilifi pia wameanza kupaka rangi nyeusi kwenye nywele zao ili wasiitwe wachawi na kuuawa.

“Tangu lini nywele nyeupe zikawa ishara ya uchawi? Hata mimi niko nazo na tunasema mvi ni upeo wa maisha ya mtu. Tusiwauwe wazee. Kwanza Kinango ndilo eneo hatari sana kwa wazee wenye mvi. Tunahitaji wazee ndiposa hata serikali inawalipa kila mwezi kwa kuwa ni mzee,” Bw Elungata alisisitiza.

Mwaka uliopita, zaidi ya wazee 60 katika kaunti za Kwale na Kilifi waliuawa kwa tuhuma za uchawi na masuala ya ardhi.

Mauaji hayo ya kiholela yalisababisha ujenzi wa sehemu ya kuokoa wazee ambao wanashukiwa kuwa wachawi wanakohifadhiwa katika sehemu ya Ganze, Kaunti ya Kilifi.

Zaidi ya wazee 87 wamewahi kutorokea makao hayo baada ya kushukiwa kuwa wachawi.

Kwa sasa kuna wazee tisa ambao wanahifadhiwa katika sehemu hiyo baada ya kuponea vifo.

Kulingana na mwenyekiti wa kituo hicho, Bw Emmanuel Katana, ukosefu wa chakula, maji ni baadhi ya changamoto zinazokumba makao hayo.