Wazee wakemea wanasiasa kwa kuvuruga Mumias

Wazee wakemea wanasiasa kwa kuvuruga Mumias

NA SHABAN MAKOKHA

WAZEE kutoka Mumias wamekasirishwa na wanasiasa kufuatia kauli wanazotoa kuhusiana na Kampuni ya Sukari ya Mumias ambayo imekuwa imefilisika na kufungwa kwa miaka minane.

Wakiwa katika Baraza la Wazee wa jamii ya Wanga wamewataka wanasiasa kutojihusisha na masuala ya kampuni hiyo na kumpatia muda mwekezaji anayejaribu kuifufua.

Walisema kwamba kauli za wanasiasa zinatishia uthabiti wa shughuli za kiwanda hicho.

Ingawa baraza hilo halina ushawishi katika kufanya maamuzi muhimu kwa jamii, wazee hao wanaheshimiwa katika jamii.

Wanasiasa, wa eneo hilo na kitaifa, wamekuwa wakizozana kuhusu kufufuliwa kwa kiwanda hicho kilichofilisika huku kila upande ukilaumu mwingine kwa kuzuia kufufuliwa na ustawi wake.

Hata hivyo, wote wanaahidi kukifufua wakichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Jumanne ijayo.

Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One KenyaRaila Odinga na mpinzani wake mkuu katika muungano wa Kenya Kwanza William Ruto wameahidi kwamba watahakikisha Mumias inafufuliwa iwapo watashinda uchaguzi na kuunda serikali.

Bw Odinga alifufua siasa za sukari katika kaunti ya Kakamega alipotambulisha meneja wa Sarrai Group, iliyopatiwa kandarasi ya kukodisha mali ya Mumias katika mkutano wa kisiasa uliofanyika uwanja wa michezo wa Bukhungu Desemba 31 2021.

Alisema kwamba kufufuliwa kwa kiwanda hicho kutakuwa jukumu la kwanza la serikali yake ili kiweze kubuni nafasi za ajiira kwa vijana na kulelea wakazi mapato.

Dkt Ruto alisema kwamba atahakikisha kiwanda hicho kitafufuliwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuunda serikali akishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto alimlaumu Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake wa handisheki, Bw Odinga kwa kushindwa kufufua Mumias.

Mara kadhaa, Bw Odinga amemlaumu seneta wa Kakamega Cleophas Malala kwa kutumiwa na kampuni hasimu kuhujumu kufufuliwa kwa Mumias.

Mnamo Juni 2021, Seneta Malala aliingilia kati na kusimamisha kukodishwa kwa Mumias kwa kampuni ya Devki akitoa matakwa makali kwa wanaotoka kukodisha kiwanda hicho.

Devki ilijiondoa ikitaja mazingira yasiyofaa, hatua ambayo ilipandisha joto la kisiasa eneo la Magharibi huku viongozi wakirushiana lawama.

Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Wanga Bw Andrew Okumu alisema kwamba wakazi hawafurahishwi na juhudi zinazoendelea za Sarrai Group za kufufua kiwanda hicho na akawataka wanasiasa kujitenga ma masuala ya Mumias.Alisema kwamba familia nyingi zinateseka katika umasikini kwa kuwa kiwanda hicho kilifilisika na kusitisha shughuli zake.

“Mumias iliporomoka kwa sababu ya siasa mbaya na hatutaki kuona wanasiasa wakiingilia masuala ya kiwanda hicho tena. Wanasiasa wanafaa kupatia mwekezaji mpya muda wa kufufua kiwanda hicho kwa sababu kinategemewa na mamilioni ya watu,” akasema Bw Okumu.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sote tuwe washindi katika kura juma lijalo

DPP aamuru polisi kuchunguza video ya uchochezi

T L