Habari Mseto

Wazee walaani mazoea ya viongozi Kisii kurushiana cheche mazishini

February 16th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

BARAZA la Wazee kutoka Jamii ya Abagusii (ACDC), limelaani vikali mazoea ya baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo kugeuza hafla za mazishi kuwa majukwaa ya kupimana nguvu kuhusu ubabe wao.

Baraza hilo badala yake limewaomba viongozi waliochaguliwa kutumia nafasi wanazopewa mazishini kufariji familia zilizofiwa kwa kusema maneno ya kuwatia nguvu.

Haya yanajiri kufuatia tukio la hivi punde ambapo Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na Gavana wa Kisii Simba Arati walitofautiana na kulaumiana vikali kuhusu uhuni ulioshuhudiwa wakati wa misa kabla ya mazishi ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu–Rasi–wa Chuo cha Kiufundi cha Kisii marehemu Daniel Nyariki wiki moja iliyopita.

Kwenye hafla hiyo, Bw Machogu alikuwa akisoma hotuba ya Rais William Ruto kwa waombolezaji gavana Arati alipoingia na wafuasi wake.

Wafuasi hao wengi wao wakiwa wahudumu wa pikipiki, walianza kumshangilia Bw Arati alipokuwa akiingia na waziri Machogu akalazimika kusitisha usomaji wa hotuba ya rais mara si moja.

Akionekana kukerwa na hali hiyo, Bw Machogu alimnyooshea Bw Arati kidole cha lawama na kumtuhumu kwamba alikuwa amewalipa vijana hao ili wamshangilie mazishini.

Hata hivyo, Bw Arati alikana kuwalipa vijana hao na alimjibu Bw Machogu kwa kumdhihaki kuwa alimshinda kinyang’anyiro cha ugavana wa Kisii na lau sio rais kumuonea huruma na kumteua serikalini, angekuwa anaumia kwa kijibaridi.

Taswira iliyoshuhudiwa mazishini humo ilivutia baraza hilo la wazee hao ambao wamejitokeza kulaani tabia za wanasiasa kuteka hafla za mazishi na kuzifanya majukwaa ya kujibizana.

Akiongea baada ya kikao na wazee wengine mnamo Ijumaa, mwenyekiti wa baraza hilo Araka Matundura alikosoa mazoea ya viongozi kulumbana kila mara na kusema cheche zinaharibia jamii jina.

“Mazishi huwa hafla ya kufariji familia na ni sherehe za kitamaduni. Si za kupimana nguvu jinsi tunavyoona kwa sasa katika mazishi. Tunakemea tabia hiyo na tunaamuru ikome,” Bw Matundura alisema.

Aliongeza, “Unapopata fursa mazishini, sema pole au taja uhusiano wako katika familia iliyofiwa au jinsi mlivyojuana na marehemu. Mambo mengine zaidi ya hayo, tafuteni majukwaa mengine.”

Baraza hilo lilisikitikia hali za wanasiasa kufokeana, kuitana majina na hata kufikia mahali ambapo wanarushiana makonde mbele ya waombolezaji. Walilaani hatua za aina hiyo.

Ili kudhibiti hali, baraza hilo limetaka viongozi kukoma kupiga siasa za aina yoyote mazishini na kutowasafirisha wahuni kwa minajili ya kuwashangilia au kuwazomea wapinzani wao.

Bw Matundura aliwasihi watu wote kuwaheshimu watu ambao wameaga dunia.

“Mazishi si mahali pa kudondoa ajenda zako za maendeleo ya ajabu,” alisema Mwenyekiti.